
Dar es Salaam. Kiwanda cha kuunganisha magari nchini cha GFA kilichopo Kibaha mkoani Pwani, kimeibuka mshindi wa kwanza kwa kampuni za kati nchini, kwenye tuzo za Rais kwa wazalishaji bora (PMAYA), zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zilitolewa jana Novemba 8, 2024 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyetoa rai kwa wazalishaji wa viwandani kuongeza wigo wa uwekezaji katika viwanda vya kimkakati vinavyozalisha bidhaa za kati, hususan vile vinavyozalisha ajira kwa wingi, kuchochea ubunifu, tija na vyenye uhusiano mkubwa na sekta nyingine.
Dk Mpango amesema kwa sasa viwanda vinafanya vizuri kiasi katika kuzalisha bidhaa za walaji, vinywaji, vyakula, bidhaa za ujenzi hususan saruji, nondo, marumaru na mabati. Hata hivyo, viwanda hivyo bado vinategemea sehemu kubwa ya malighafi zake kutoka nje.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Ezra Mereng amesema lengo na kiu yao ni kuhakikisha wanaendelea kuongoza kwa kuzingatia ubora na viwango vya uunganishaji magari nchini.
“Ubora ndiyo silaha kuu ya ushindi wetu, tunaahidi kuliendeleza hilo na kuongeza ubunifu zaidi,” amesema.
Amewapongeza wafanyakazi akisema wao ndio chachu ya mafanikio na kukidhi ubora katika uzalishaji wa magari, ikiwa ni mara ya tatu wanapata ushindi.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Salman Karmali amesema tuzo hiyo inaonyesha wanasimamia malengo ya uanzishwaji wa kampuni wakiwa na deni la kuwapatia wateja kila wanachotarajia.
Amesema kutokana na imani yao kwa wateja na nchi kwa ujumla, wanaanza awamu ya pili ya upanuzi na uzalishaji wakitarajia kuunganisha magari makubwa 10 kwa siku kutoka magari manne waliyokuwa wakiunganisha awali.
“Upanuzi huu utatuwezesha kulifikia soko la ndani na nje ya nchi hasa ukanda wa Afrika Mashariki, ambako mbali na manufaa yetu kama kampuni, pia tutaliingizia Taifa fedha za kigeni,” amesema.
Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanawawezesha Watanzania kufanya kazi katika miradi ya Serikali ambayo huwawezesha kununua mahitaji muhimu binafsi na ya kuendesha miradi.