Miili ya wanakwaya sita Same yaagwa, kuzikwa kesho Chome

Same. Miili sita ya wanakwaya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mmeni Chome, Dayosisi ya Pare waliofariki kwa ajali ya gari wilayani Same mkoani Kilimanjaro imeagwa leo Aprili Mosi, 2025.

Ajali hiyo ilitokea Machi 30, 2025 eneo la barabara ya Bangalala, wakati wanakwaya hao wakitokea Chome kuelekea Vudee kuinjilisha.

Gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Coaster lilikosa mwelekeo na kupinduka katika milima ya Pare na kusababisha vifo hivyo na majeruhi 23.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Namsifu Mbula (79), Mbazi Mjema (14), Paulo Mchome (40), Christina Kirumbi (60), Agness Mchome (59) na Niwaeli Ngeruya (74).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na dayosisi hiyo, ibada ya mazishi itafanyika kesho Aprili 2, 2025 katika Usharika wa Chome.

Miili ya wanakwaya hao imeagwa leo Aprili Mosi, 2025 katika kanisa kuu la KKKT, Dayosisi ya Pare.

Mkuu wa dayosisi hiyo, Askofu Charles Mjema akihubiri katika ibada ya kuaga miili hiyo amewataka wananchi kuishi maisha ya kujiandaa wakati wote na kuacha dhuluma.

“Katika maisha yetu hapa duniani tuishi kama tunaokufa sasa hivi, maana hatujui wakati wa bwana utafika lini. Tuache kuishi maisha ya kiholela, ya kujifikiria kuwa tutakaa hapa duniani, unajua wale wanaowadhulumu wenzao wanafanya hivyo kwa sababu wanafikiri wana maisha marefu, lakini unaweza ukamdhulumu leo na baadaye ukawa haupo.”

“Acha dhuluma, ndugu zangu, maisha yetu ni mafupi mno na kwa kuwa siri hii imefichwa hakuna anayejua muda na saa ya kuondoka duniani. Bwana anasema uwe tayari wakati unaofaa na usiofaa, tengeneza mambo yako ili ikitokea kuitwa ufie mikononi mwa Bwana,” amesema.

Askofu Mjema amesema wanakwaya hao walikuwa wanakwenda Usharika wa Vudee kutoa sadaka kwa ajili ya huduma za misioni.

“Wanakwaya hawa walikuwa wamealikwa kwa ajili ya kushiriki kutoa sadaka muhimu ya misioni. Ndani ya dayosisi yetu tuna sadaka ya misioni inayotumika kueneza injili katika maeneo yale ambayo kipato chao ni kidogo ili watumishi wanaotumika pale waweze kueneza injili,” amesema na kuongeza:

“Walikuwa wamejiandaa vizuri kwa sadaka hiyo wakiwa na mchungaji wao ndani ya gari ambaye alikuwa wa kwanza kutupwa nje, hakupona kwa sababu ni mwema sana mbele za bwana, hapana! Mungu ana makusudi akafanyike kuwa ushuhuda kwa watu wote hata katika mazingira magumu Mungu anaweza.”

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali imepoteza watu muhimu katika jamii, akataka kila mmoja kuishi maisha yanayompendeza Mungu wakati wote.

“Taarifa hizi tulizipokea kwa mshtuko, kikubwa tunachojifunza katika maisha haya, hatuna uhakika na maisha yetu hapa duniani.  Hatujui saa, dakika wala siku, ndugu zetu hawa waliamka Jumapili wanakwenda kwenye kanisa jingine kwa ajili ya ibada lakini siku yao Mungu aliyowapangia ikawa imefika,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amesema Serikali itaendelea kuhakikisha majeruhi wanapata matibabu bila kujali wana fedha au hawana.

“Tutajitahidi kushirikiana na kanisa kuhakikisha tunaokoa roho za majeruhi, ikumbukwe kulikuwa na ajali mbili, moja ilitokea usiku ambayo majeruhi walikuwa 52 wakati nahangaika kuokoa uhai wa majeruhi hawa tukapata tena taarifa ya kuondokewa na watu sita na majeruhi 23, inaumiza sana lakini niendelee kutoa pole kwa kanisa na familia ambazo zimeondokewa na wapendwa hawa,” amesema.

Mbunge wa Same Magharibi, David Mathayo ameishukuru Serikali kwa namna inavyowahudumia majeruhi.

“Familia zilizopoteza wapendwa wetu kwa sababu suala la msiba ni la dharura na hakuna aliyejiandaa, ningependa kuwashika mkono kwa Sh2.4 milioni ambazo kila familia itapata Sh400,000,” amesem

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *