Maafisa wa Libya wamegundua kaburi la pamoja katika wilaya ya Kufra, likiwa na miili ya watu 28 ambao ni wahamiaji waliokuwa wanapitia nchi hiyo kwenda barani Ulaya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali nchini Libya, imethibitisha kupatikana kwa miili hiyo na kueleza kuwa watu hao waliteswa na kuzuiwa na baadaye kupoteza maisha, kabla ya kuzikwa pamoja.
Tukio hili linaelezwa kuwa lilitokea Jumamosi iliyopita, katika eneo maarufu ambalo wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika hupitia wakilenga kutumia usafiri wa majini kupitia bahari ya Mediterranean kwenda katika mataifa ya Ulaya.

Aidha, imebainika kuwa kundi la wahamiaji hao walivamiwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama kabla ya kuuawa na miili yao imeonekana ikiwa na majeraha mabaya, na tayari raia mmoja wa Libya na wawili wa kigeni wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Jumuiya ya Kimataifa, ikiwemo Tume ya Umoja wa Mataifa ya kuwaisaida wahamiaji IOM imekuwa ikiishtumu Libya kwa kuwatesa watu hao na kwenda mbali kuwafanya kuwa watumwa.
Mwezi Machi mwaka uliopita, kaburi lingine la pamoja lilibainika likiwa na miiili ya wahamiaji 65 Kusini Magharibi mwa nchi hiyo kwa mujibu wa Tume ya Umoja wa Mataifa IOM.