Miili tisa yahifadhiwa Amana, wengine wawili waokolewa Kariakoo

Dar es Salaam. Miili tisa kati ya 15 iliyoagwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jana Jumatatu, Novemba 18, 2024 imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Amana ikisubiri utaratibu wa ndugu kuichukua kwa ajili ya maziko.

Jumla ya watu 16 wamefariki dunia kwa kuporomokewa na ghorofa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, saa tatu asubuhi Novemba 16, 2024. Jengo hilo limesababisha majeruhi 86 na hasara ya mamilioni ya fedha.

Shughuli ya kuiaga miili hiyo 15 kati ya 16 ilifanyika jana Jumatatu, Uwanja wa Mnazi Mmoja ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, ndugu, jamaa na marafiki wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Pia, shughuli ya kuwaokoa wengine waliosalia kwenye jengo hilo, inaendelea leo Jumanne, Novemba 19, 2024, huku Rais Samia Suluhu Hassan akimuelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuongeza saa 24 ya kufanya kazi hiyo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu natambua utaratibu wa uokoaji una muda maalumu wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kutenda miujiza yake na kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamekwama kwenye jengo hilo. Ninatoa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kupambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai,” amesema Rais Samia.

Mapema asubuhi ya leo Jumanne, Mwananchi imefika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana kujua kinachoendelea kwa miili hiyo. Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bryceson Kiwelu amesema baada ya shughuli ya kuaga jana, miili tisa imerudishwa kuhifadhiwa hospitalini  ikiwa ni maombi ya ndugu.

Dk Kiwelu amesema ndugu hao wameomba iwe hivyo wakisubiri ndugu zao wengine ambao bado hawajapatikana hadi sasa.

“Baadhi ya ndugu wameomba tuendelee kuhifadhi miili ya wapendwa wao hapa, wakisubiria hatima ya kupatikana kwa wengine waliokuwa kwenye jengo hilo,” amesema.

“Katika msiba huu kuna wanandugu wengine wanasafirisha miili kupeleka mkoani, nadhani pia hii inaweza kuwa sababu kutaka kuona kama kuna mwingine utapatikana wasafirishe au kuzika kwa pamoja hata kama maziko yatafanyikia hapa hapa Dar es Salaam,” amesema daktari hiyo.

Mwananchi imeshuhudia ndugu, jamaa na marafiki wakiwa hospitalini hapo wakisubiri kupata utaratibu mwingine.

Wengine wawili waokolewa

Wakati ndugu wa Mery (Maria) Lema wakishinda usiku na mchana kujua hatma ya ndugu yao ambaye wanadai ni miongoni mwa walionasa kwenye kifusi cha jengo hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Thobias Makoba amesema watu wengine wawili wameokolewa usiku wa jana na leo asubuhi.

Amesema watu hao, wapo hospitali kwa matibabu huku shughuli ya uokozi ikiendelea hadi watakapomfikia mtu wa mwisho aliyenasa katika jengo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa eneo hilo, Makoba amesema uokozi ambao umekuwa ukikosolewa na baadhi ya watu kwamba unakwenda polepole hauna uhalisia kwa kuwa,  kutoa vifusi na kuwafikia watu walionasa kunahitaji weledi wa hali ya juu na halifanyiki taratibu kama wengi wanavyodhani.

“Changamoto kubwa ambayo watu wengi hawaijui na wakifika hapa wataelewa, sio kama uokozi unakwenda taratibu, lakini kwa namna ambavyo jengo lilivyoanguka huwezi kuchukua greda ukachota tu visufi ukakitoa,” amesema Makoba ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.

“Kwa namna lilivyoanguka linahitaji ustadi mkubwa ili kuhakikisha wale wenzetu waliokamatika kule chini, hatutengenezi mazingira ya jengo kuanguka tena na kuwamalizia. Ndio maana wanavyochoronga ni taratibu na weledi, ukitumia nguvu litaanguka,” amesema.

Akieleza namna walivyoweza kuwasiliana na kuwafikishia hewa safi, maji na glucose watu walionasa chini ya kifusi na kushindwa kuwatoa kwa haraka baada ya mawasiliano, Makoba amesema, saizi ya tundu linalotumika kupeleka mawasiliano kwa watu hao halizidi sentimita 3.

“Wanachokifanya wataalamu wetu wa uokozi, kwanza ni kumsikia huyo mtu, kisha kumpa msaada wa maji, hewa na glucose na kisha ndipo wanaangalia namna ya kumsaidia,” amesema.

Alivyowasiliana na ndugu yake

Wakati shughuli za uokozi zikiendelea, baadhi ya ndugu wanasema wamelazimika kukesha eneo hilo tangu Jumamosi kusubiri hatima ya ndugu yao waliyemtaja kwa jina la Mery Lema ambaye wanadai ni miongoni mwa walionasa kwenye jengo hilo hadi kufikia leo saa 4:00 asubuhi.

“Tulikuwa tukiwasiliana naye hadi jana mchana, alitupigia akiomba msaada, kikubwa alichokilalamikia yeye (Maria) ni hewa, leo tumejaribu kuipiga simu yake haipatikani,” amesema mdogo wa Mery bila kutaka kutaja jina lake.

Amesema dada yake alikuwa na duka la nguo katika jengo hilo na wakati akiwasiliana naye, alimwambia yupo na wenzake wanane, hivyo jumla walikuwa tisa, tuwaombeeni tu watoke salama,” amesema.

Endelea kufuatilia Mwananchi