Rukwa. Miili tisa ya wavuvi waliokumbwa na dhoruba katika bonde la ziwa Rukwa imetambuliwa majina huku taratibu za kuwatafuta ndugu zao zikiendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile leo Januari 26,2024 ametaja miili iliyotambuliwa majina kwa mujibu wa wavuvi wenzao walionusurika kwenye dhoruba hiyo kuwa ni Omary Ngasa,Adolf Charles, Conrad Cassian, Emmanuel Mkandawili, Baraka Mhagama, Emmanuel Sime, Amosi Isaya, James Simponzi na Ngosha ambaye bado hajapatikana.

Chirukile amesema miili ambayo imetambuliwa kwa majina lakini ndugu zao hawatambuliki Serikali itatoa utaratibu wa mazishi.
Amesema juhudi za kutafuta mwili wa Ngosha bado zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vikosi vya jeshi la zimamoto na uokoaji.

Pia amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki huku wakiendelea kuchukua tahadhari kulingana na utabiri unaotolewa na mamlaka ya hali ya hewa.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Rukwa, Chacha Mchaka amesema mapema asubuhi ya leo wapambanaji waliingia ziwani ili kuendelea na juhudi za kutafuta mwili wa mvuvi mmoja, aliyefahamika kwa jina la Ngosha.
Mmoja wa wavuvi walionusurika kwenye dhoruba hiyo, Mashaka Elias amesema wanaishukuru Serikali kwa jitihada kubwa za uokoaji uliofanyika na anaamini mwili wa Ngosha utapatikana.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu mimi na wenzangu tulitoka salama tunawaombea wenzetu waliotangulia mbele ya haki pia naipongeza sana Serikali kwa kufika kwa wakati na kutoa msaada,” amesema.