
Dodoma. Miili ya watu wanane waliofariki dunia katika ajali ya basi la AN Classic linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kigoma imetambuliwa, huku majeruhi waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wakiendelea vizuri.
Akizungumza leo Machi 5,2025 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi amesema kuwa majeruhi 26 waliopo hospitalini hapo wanaendelea vizuri.
“Matarajio yetu tutawaruhusu wengine baada ya kuona hali zao zinazidi kuimarika,” amesema Dk Ibenzi.
Hadi kufikia jana Machi 4,2025 watu wanane walifariki dunia huku wengine 55 wakijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea Chigongwe, mkoani Dodoma, saa 4.00 usiku wa Machi 3,2025.
“Tangu jana hatuna kifo chochote ambacho kiliongezeka, tunamshukuru Mungu na madaktari wanaendelea kupambana ili kuokoa maisha ya hawa ndugu zetu,” amesema Dk ibenzi.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani katika kipindi cha kati ya Julai hadi Septemba 2024, watu 453 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani.
Idadi hiyo ya vifo imepungua kutoka 477 vilivyotokea katika kipindi kama hicho mwaka 2023 huku waliojeruhiwa wakiwa ni 835, ikilinganishwa na 782 wa mwaka 2023.
Vyanzo vya ajali vikitajwa kuwa ni mwendo kasi, matumizi ya vilevi, miundombinu, kutokuzingatiwa kwa aheria za usalama barabarani, matatizo ya kiufundi na uzembe wa madereva.