Migogoro ya ardhi yatikisa mjadala bajeti ya Ardhi, watendaji wa Serikali watajwa

Unguja. Wakati Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ikiliomba Baraza la Wawakilishi kuipitishia Sh345.4 bilioni kutekeleza vipaumbele vinane, wajumbe wameitaka Serikali iweke mipango ya kupima ardhi ili kuondosha migogoro, ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watendaji wa Serikali.

Pia, wamesema licha ya nia njema ya Serikali, wananchi wanalalamika kutolipwa fidia na wengine kulipwa kiasi kidogo baada ya nyumba zao kuvunjwa kupisha miradi.

Wameeleza hayo leo Jumatatu, Mei 19, 2025, wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika mkutano wa 19 wa Baraza hilo, Chukwani, Unguja.

Mwakilishi wa Kwahani, Yahya Rashid Mamba amesema bado kuna migogoro mingi inayosababishwa na watendaji wa Serikali, hivyo wizara inapaswa kusimamia hatua hiyo.

“Bado ardhi inahitajika Zanzibar, lakini migogoro imekuwa mikubwa na migogoro hii wapo viongozi wanaotajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa. Lazima ziwekwe sheria ambazo zitasimamia tatizo hili na viongozi hawa wasiwe chanzo cha migogoro,” amesema Mwakilishi huyo.

Naye Mwakilishi wa Paje, Dk Soud Nahoda Hassan amesema bado Zanzibar haijawa na mpango mzuri wa ardhi, hali inayoibua ujenzi holela na kusababisha migogoro, hivyo kuitaka wizara kuharakisha mpango wa kupanga miji.

Amesema ardhi haiongezeki, watu wanaongezeka, hivyo wizara ijipange kujenga nyumba zinazojengwa juu.

Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema wizara hiyo inagusa hali za watu wengi, na Serikali imesahau kuwa ardhi ni mali ya umma, badala yake imejitwalia mamlaka na kuibua migogoro kwenye jamii.

Amesema migogoro mingi inasababishwa na viongozi wa Serikali wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya na masheha kwa maslahi binafsi.

“Viongozi wa Serikali wasijiingize kwenye migogoro hii, wamekuwa sehemu kubwa ya migogoro,” amesema.

Hamad amesema mipango ipo, lakini changamoto ni utekelezaji, akikumbushia kuwa mpango wa kupima ardhi ulianza tangu mwaka 1992, ukiahidi kukamilika ndani ya miaka mitano, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika, hali inayochochea migogoro hiyo.

Amesema kuna watu wananufaika na migogoro hiyo na ndiyo maana inakuwa vigumu kukamilisha mipango ya upangaji wa ardhi, hali inayoendelea kuleta chuki kwa wananchi.

Hamad amezungumzia kuhusu nyumba za makazi, akisema zinapaswa kujengwa kwa lengo la kuwahudumia watu wa hali ya chini, hasa watumishi wa kipato kidogo, lakini nyumba zinazojengwa hazina sifa za kuitwa za bei nafuu.

Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu amesema chanzo cha migogoro hiyo ni kutokuwa na mifumo imara ya kuweka kumbukumbu, hivyo kila mmoja kufanya anavyotaka.

“Kuna hati feki nyingi za ardhi na hilo ndilo linalochangia migogoro. Kwa hiyo, tutengeneze mifumo ambayo itasaidia kuepusha changamoto hii,” amesema.

Hamad amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar imekumbwa na migogoro mikubwa ambayo haitakwisha, ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Akizungumzia kuhusu fidia, Makungu amesema jambo hilo nalo linaibua chuki kwa wananchi wanaohamishwa kupisha miradi, lakini hawalipwi fidia baada ya nyumba zao kubomolewa.

“Hili ni jambo jema, miradi inatusaidia, lakini wananchi wanaopisha miradi hawalipwi fidia. Inaibua chuki kwa wananchi na wengine wanaishia kuombea dua mbaya. Sasa Serikali lazima ilione hili,” amesema.

Mwakilishi wa Uzini, Haji Shaaban Waziri amesema licha ya Serikali kusema inajenga nyumba za bei nafuu, kiuhalisia hazina nafuu, badala yake zinawanufaisha wenye uwezo na kuwaacha watu wa kada ya chini wakiangaika.

Awali, akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri wa Ardhi, Rahma Kassim Ali amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26, wizara hiyo imejipanga kutekeleza vipaumbele vinane, ikiwemo kuendelea na ujenzi wa nyumba mpya za makazi na biashara pamoja na kufanya matengenezo ya nyumba zilizopo.

Pia, kuendelea na ujenzi wa mifumo ya utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta ya ardhi na makazi, na kuendelea na utambuzi wa ardhi pamoja na uandaaji wa mipango mikuu na ya kina ya matumizi ya ardhi ya miji mbalimbali Unguja na Pemba.

“Kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya ardhi na makazi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” amesema Waziri.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Yahaya Rashid Abdulla amesema kamati imebaini kuwa migogoro mingi inachangiwa na mipaka, eneo moja kuuzwa zaidi ya mtu mmoja, uvamizi wa maeneo ya wazi na kuongezeka kwa thamani ya ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *