Migogoro ya ardhi inavyozaa matukio ya jinai

Dar es Salaam. Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amesema migogoro ya ardhi ndio inayozaa makosa mengi ya kijinai nchini, sambamba na kuwa chimbuko la changamoto katika uwekezaji, biashara na mirathi.

Profesa Juma aliyasema hayo leo Jumatatu, Februari 3, 3035, alipozungumza katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria, ambayo kitaifa yalifanyika katika Jiji la Dodoma, huku mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hoja yake hiyo, amesema iwapo suala la ardhi litawekwa vizuri, litasaidia kutatua matatizo mengi na hata Mahakama itakuwa na migogoro michache huku mingi ikiiishia kwenye usuluhishi.

“Katika uzoefu wetu tumeona kwamba, migogoro ya ardhi ndio inazaa jinai nyingi, ni chimbuko la changamoto kwenye uwekezaji, biashara, mirathi na maeneo mbalimbali,” amesema.

Kwa sababu hiyo, amependekea suala la ardhi kuhitaji uangalizi wa hali ya juu katika Dira ya Taifa mwaka 2050, inayoendelea kuandaliwa.

“Hili ni eneo ambalo sisi Mahakama tunaliona lina umuhimu wa pekee,” alisema.

New Content Item (1)

Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe  Februari 03, 2025.

Hoja iliyoibuliwa na Profesa Juma iliongezewa nguvu na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Enos Misana aliyesema migogoro ya ardhi ndio inayolalamikiwa zaidi na wananchi wilayani humo.

Katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria wilayani humo, Misana amesema baadhi ya wananchi wanadhulumiana kwa kupeana mikataba isiyo ya kisheria.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwatumia wanasheria wanapouza na kununua ardhi ili kupunguza migogoro hiyo.

“Migogoro ya ardhi ndilo eneo ambalo linaonekana kuwa na changamoto kubwa wakati tukitoa elimu ya sheria katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu, hivyo sisi Mahakama tumejipanga na kuhakikisha kuwa shughuli ya utoaji elimu ya kisheria kwa umma inakuwa endelevu,” amesema.

Sambamba na ardhi, amesema migogoro mingine ni mirathi na ndoa.

Mfano halisi wa hilo ni Antoni Mkune mkazi wa kijiji cha Nguliguli wilayani humo, aliyesema amekuwa akisumbuka muda mrefu kupata haki yake baada ya kunyanganywa shamba aliloachiwa na wazazi wake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Nimehangaika muda mrefu kutokana na  eneo ambalo lilichukuliwa kiujanja ujanja. Nimekwenda ofisi mbalimbali lakini sijapata msaada wowote ila sasa baada ya kufika hapa mahakama ya wilaya, nitaonana na hakimu ilia anieleze nianzie wapi ili nipate haki yangu,” alisema.

Shida iko hapa

Sheria iliyoipa rasilimali hiyo hadhi ya kuwa bidhaa na kuifanya kuwa moja ya dhamana iwapo mtu atahitaji kukopa fedha benki, ndio mzizi wa tatizo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utetezi wa Haki za Ardhi (Hakiardhi), Cathbert Tomitho kabla ya sheria iliyopo sasa, ardhi haikuwa bidhaa na haikuwa rahisi kuiuza kwa Sh1 bilioni.

Kilichokuwa kinauzwa wakati huo, amesema ni maendeleo yaliyofanywa katika ardhi husika, mathalan kama kuna nyumba hicho ndicho kinachouzwa.

“Kwa hiyo ilikuwa ukinunua nyumba ndipo unapata na ardhi au ukinunua mimea au miti ndio unapata na ardhi,” amesema Tomitho, alipozungumza na Mwananchi.

Lakini ilipokuja sheria ya ardhi ya mwaka 1999, amesema ilitambulisha soko la ardhi na msukumo huo uliwekwa na taasisi za fedha zilizoibainisha kuwani  moja ya dhamana za kupatia mikopo.

Kuanzia hapo, amesema ardhi ikapewa thamani ya fedha na ndipo migogoro ilipoanzia.

Hali hiyo kwa mujibu wa Tomitho, imesababisha wachache wamiliki maeneo makubwa bila kuyaendeleza huku wakisubiri yapande thamani ili wauze kwa bei kubwa.

Sambamba na hilo, sababu nyingine ameitaja ni kukosekana kwa utaratibu mzuri wa usimamizi katika eneo la uuzaji na ununuzi wa ardhi, kwani imebaki biashara holela iliyokosa udhibiti.

“Ukija kwenye ardhi hakuna mdhibiti kuna kiwanja cha bilioni moja na kuna kingine hapohapo cha bilioni 10,” amesema.

Alieleza matajiri kwa sasa wamewekeza fedha zao katika ardhi, kwa sababu wanajua ndiko fedha ziliko na masikini wanabaki kuteseka.

Ili kutatua changamoto iliyopo, alipendekeza ufanyike utafiti kupitia tume itakayoundwa, kubaini chanzo cha kesi nyingi za jinai na hata za madai katika sekta ya ardhi.

Utafiti huo, amesema uhusike pia kuangalia namna mfumo wa umiliki, uuzaji, ununuaji, ugawaji wa ardhi unavyosimamiwa na kisha itoe mapendekezo.

Hayo, amesema yaambatane na marekebisho ya sheria ili kuundwe mamlaka ya usimamizi wa uuzaji wa ardhi itakayodhibiti bei.

‘Samia, Mwabukusi lugha moja’

Katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka majaji na mahakimu wa mahakama mbalimbali, kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano ya kisheria na kikatiba, badala ya kuwa ‘miunguwatu’.

Alilifafanua neno miunguwatu, akilihusisha na binadamu wanaotekeleza wajibu wao kwa kujipa ukubwa unaofanana na ule wa Mwenyezi Mungu, jambo alilosema watumishi wa taasisi za haki jinai na madai hawapaswi kuwa nalo.

Hata hivyo, Rais Samia ameitoa kauli hiyo kukazia kile kilichoibuliwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi ambaye awali aliwataka mahakimu na majaji wasitengeneze mazingira ya kuchelewesha kesi mahakamani.

 “Kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu, ambayo mbali ya kutoa haki ana kudra na jaala, anaweza kuamua akupe au akunyime sasa hiyo ni kazi ya Mungu,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wa majaji na mahakimu, alisema wao ni mawakala wa utoaji haki duniani, lakini mmenyimwa jaala na kudra hivyo hawana uwezo wa kuamua kutoa au kumnyima binadamu.

“Kwa hiyo mnafanya kazi yenu kwa kufuata makubaliano yetu kikatiba na sheria za nchi kama tulivyoziweka,” alisema.

Kwa sababu hiyo, aliwataka wasiwe miunguwatu kwa kuwa hawana jaala wala kudra, hivyo watoe haki kwa kufuata misingi waliyokubaliana na iliyowekwa kisheria na kikatiba.

Aliwasisitiza wanapouanza mwaka mpya wa mahakama, wadhamirie kukaa upande wa haki na waizingatie wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Aliyasema hayo akirejea hotuba ya mwaka 1984 iliyowahi kutolewa na Mwalimu Julius Nyerere aliyewaambia majaji kuwa kazi yao inahitaji uadilifu na nidhamu isiyotiliwa shaka.

Mkuu huyo wa nchi alitumia jukwaa hilo, kujibu hoja mbalimbali za Mwabukusi ikiwemo maboresho ya maslahi ya mahakimu, akisema linaendelea kufanyiwa kazi.

“Maombi haya yalikuja katika mwaka huu wa fedha hayakuwa kwenye bajeti tumejitahidi kubana na kuanza na yale yanayowezekana kuanza, lakini mengi yatakuja Julai mwaka huu wakati wa bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja,” amesema.

Amesema anafanya namna kuhakikisha wanauwezesha mfuko wa TLS ili itekeleze majukumu yake bila changamoto.

Kwa kuwa Mwabukusi ameahidi kuendelea kupokea msaada wowote utakaowezesha kutekeleza wajibu wa TLS, Rais Samia amemwambia ataangalia linalowezekana kukipatia chama hicho gari lingine, mbali na lile lililotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria.

‘Hatujalamba asali’

Kwa upande wake, Mwabukusi ametumia jukwaa hilo kuweka wazi kuwa ushirikiano wa chama hicho na Serikali,  hauna maana kuwa amelamba asali, bali wanatekeleza wajibu wa kuwahudumia Watanzania.

Kauli hiyo ya Mwabukusi inajibu mitazamo tofauti inayoibuliwa katika mitandao ya kijamii, baadhi wakikosoa hatua ya TLS kushirikiana na Serikali katika utoaji huduma za kisheria kupitia Samia Legal Aid.

Kadhalika, ukosoaji mwingine uliohusisha madai ya kulamba asali, ni hatua ya chama hicho kupewa gari na Wizara ya Katiba na Sheria.

“Tunaposhirikiana na Serikali hatulambi asali, kwa sababu tunapata changamoto watu wanapoona tunashirikiana na Serikali wanafikiri tunalamba asali.

“TLS sio kikundi cha magaidi ni bodi ya kisheria kwa hiyo sehemu ya kuonya tutaonya kwa haki, sehemu ya kupongeza tutapongeza kwa haki na sehemu ya kushiriki pamoja tutashiriki kulijenga Taifa letu na kumhudumia Mtanzania,” alisema.

Kuhusu gari walilopewa, alisema linawasaidia kuwafikia Watanzania na wapo tayari kupokea msaada mwingine wowote kutoka kwa yeyote ili kuwawezesha kuwafikia wananchi.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, chama hicho hakina fedha za kutosha kuwahudumia wananchi, hivyo kinahitaji kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kinatekeleza wajibu wake.

“Yeyote anayetuletea msaada tutaendelea kupokea. Popote tutakapohitaji kwenda kushirikiana na mtu kufanya kazi tutaenda kushirikiana, sio rushwa sio kutuziba mdomo, tutajitambua. TLS ina wajibu haifanyi biashara,” alisema.

Aliwajibu pia wale wanaohoji kwanini siku hizi haongei kama alivyokuwa kabla ya urais wake wa TLS akisema; “Watu wanauliza Mwabukusi huongei tena umelamba, ukishakuwa kiongozi huongei tena unatenda. Kiongozi huongei unatenda.”

Maadhimisho kwingineko

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Ilvin Mugeta akizungumza kwenye maadhimisho kama hayo mkoani Arusha, amesema taasisi za haki jinai na madai zinahitaji mabadiliko na mageuzi makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kurudi katika misingi ya kusaidia wananchi kwenye upatikanaji wa haki bila vurugu.

Amesema taasisi hizo ni muhimu kuzingatia sheria kanuni na taratibu za kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuhakikisha upatikanaji wa haki bora na kwa wakati.

Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo ameomba mahakama zote na watendaji wake, kutenda wajibu wao kwa uaminifu na uadilifu na kusimamia utolewaji wa haki bila ubaguzi.

Askofu Shoo akizungumza kwenye maadhimisho kama hayo Mkoa wa Kilimanjaro amesema: “Tunapoadhimisha siku hii ya sheria wajaalie kutambua amani katika nchi yoyote ni tunda la haki na wao wamepewa dhamana ya kusimamia haki. Mungu tunakuomba uzifanye mahakama zetu zote ziwe mahali pa kukimbiliwa badala ya kukimbiwa, kwani watu wengi watakuwa na imani nazo.”

Imeandikwa na Juma Issihaka (Dar), Sharon Sauwa (Dodoma), Samwel Mwanga (Maswa), Bertha Ismail (Arusha) na Florah Temba (Kilimanjaro)