
Mashua zimeanza tena shughuli za usafirishaji wa watu na vitu tangu siku ya Jumanne asubuhi kwenye Ziwa Kivu, kitovu cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Goma na Bukavu, miji mikubwa ya mashariki mwa DRC ambayo imeangukia mikononi mwa M23 wanaoshirikiana na wanajeshi wa Rwanda, waandishi wa habari wa AFP wamebaini.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Siku ya Jumatatu Februari 17, kundi hililinalopinga serikali lilisema katika taarifa yake kwamba “bandari zote za Goma na Bukavu zitaanza kufanya kazi saa24 kwa 24” kuanzia Jumanne. Kwa kuiteka Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, mwishoni mwa mwezi wa Januari, kisha Bukavu, mji mkuu wa jirani wa mkoa wa Kivu Kusini, siku ya Jumapili, M23 na wanajeshi wa Rwanda wamepata udhibiti kamili wa ziwa hilo.
Bukavu ilianguka bila upinzani kutoka vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARD) na shughuli zimekuwa zikiendelea katika jiji hilo tangu siku ya Jumatatu, licha ya uporaji wa maduka na maghala. Kulipopambazuka, abiria walipanga foleni kwenye bandari ya jiji la watu milioni moja ili kupanda mashua ya kwanza kuelekea Goma.
“Tuna furaha, uamuzi huu unatupa ahueni,” Lueni Ndale, mkuu wa kampuni ya usafirishaji wa watu na vitu katika Ziwa Kivu, ameliambia shirika la habari la AFP. Amehakikisha kuwa tikiti zinauzwa kati ya dola 10 na 27 kulingana na sehemu katika mashua, bei iliyoongezwa kwa kuongezeka kwa gharama ya mafuta.
Mji wa Bukavu unategemea kwa kiasi bidhaa za kilimo zinazokuzwa Kivu Kaskazini na bandari ya Goma kuzisafirisha kutokana na kukosekana kwa barabara zinazopitika kutokana na mapigano.
Abiria wengi ni wafanyabiashara ambao wamekuja kuchukua bidhaa za chakula kutoka Goma ili kuziuza katika mji pacha wa Kivu Kusini. “Maisha yalikuwa magumu kwetu, ilikuwa ngumu hata kuwa na mtu ambaye angeweza kutukopesha pesa tukiwa hatuna ajira, kwa kweli nina furaha,” anasema Amani Kalimira, mtunza mizigo.