Mifumo ya kuzuia radi muhimu kote nchini

Tukio lililotokea wiki hii katika Shule ya Sekondari Businda, wilayani Bukombe Mkoa wa Geita, limewapa changamoto kubwa wadau wa elimu kama wazazi, Serikali na jamii kwa jumla.

Tukio hilo lililohusisha mvua kubwa na radi iliyopiga darasani, lilisababisha vifo vya wanafunzi saba na majeruhi 82.

Kwa mujibu Yohana Edward, mwanafunzi aliyejeruhiwa na radi hiyo, alishuhudia wenzake wakiteketea kwa moto huku yeye akijikuta ameanguka chini akiwa na maumivu.

Tukio hilo la kiasili ni kielelezo cha udhaifu wa mifumo ya ulinzi dhidi ya radi katika maeneo ya shule na mengineyo yenye mikusanyiko, inayohitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Serikali na jamii zinapaswa kujiuliza ni kwa kiwango gani mifumo ya kuzuia radi katika shule na maeneo mengine yenye watu wengi, kama hospitali, shule na masoko, pamoja na majengo mengine binafsi, inahitajika nchini.

Tunafahamu kuwa, radi ni moja ya hatari kubwa zinazoweza kutokea wakati wa mvua kama haijadhibitiwa na madhara yake ni kifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Hivyo, ni muhimu kwa Serikali pamoja na wadau wengine, kuweka mikakati ya kuhakikisha mifumo ya kuzuia radi inapatikana katika shule zote nchini, kama alivyoshauri Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella.

Kwa mujibu wa Shigella, ripoti ya awali ya uchunguzi imebaini madarasa yaliyopigwa na radi katika Shule ya Sekondari Businda hayakuwa na mfumo wa kuzuia radi.

 Serikali itekeleze wajibu wake wa kusambaza mifumo hii kwa kuagiza mamlaka zake au kuhamasisha halmashauri za mikoa, wilaya na taasisi binafsi kuwajibika katika kuhakikisha mifumo hiyo inafungwa kwenye maeneo ya umma na mengine muhimu, hasa katika mikoa inayoathiriwa zaidi na radi.

Madhara ya kutokuwa na mifumo ya kuzuia radi yameonekana wazi katika tukio hilo; wanafunzi waliokuwa darasani walishuhudia vifo na majeraha makubwa kwa wenzao, wakati hali hii inaweza kuepukika kwa kuwepo mifumo ya kuzuia radi.

Mbali na athari za kisaikolojia kwa waliopoteza wapendwa wao, waathirika na mashuhuda, pia tunaona athari za kiuchumi kwa familia zinazopoteza watoto wao na jamii kwa jumla.

 Matibabu ya majeruhi yana gharama kubwa, na madarasa ya shule hiyo yanahitaji kurekebishwa ili kuwa salama kwa wanafunzi wengine.

 Ni jukumu la mamlaka husika, kama Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Serikali za mikoa na wilaya, kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatumika kama sehemu ya ulinzi wa maeneo ya umma.

Vilevile, taasisi za umma zinapaswa kushirikiana na wataalamu wa mifumo ya kuzuia radi ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuhakikisha kwamba mifumo hiyo inafanya kazi.

Pia, Serikali inaweza kuanzisha programu maalumu ya kutoa elimu kwa wakuu wa shule, walimu na wataalamu wa ujenzi juu ya umuhimu wa mifumo hii ya kuzuia radi, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake.

Licha ya maendeleo yanayofanyika katika sekta ya elimu, bado kuna ukosefu wa elimu hiyo, itakayowawezesha wananchi kwa sehemu kubwa, kutambua umuhimu wa mifumo hiyo ya ulinzi dhidi ya radi.

Tukio la Shule ya Sekondari Businda, kama yalivyo mengine mengi katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga na Kigoma, linapaswa kuwa fundisho kwa Serikali na jamii na kulifanyia kazi.