Mifumo ya ajira yakera wabunge

Dodoma. Wabunge wamechachamaa kuhusu utolewaji wa ajira unaofanywa serikalini wakisema umekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kimfumo huku wakihoji kinachoendelea baada ya Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda kuonesha shaka kwa baadhi ya ajira.

Wabunge hao wamehoji mfumo wa kutoa ajira unavyopeleka malalamiko mengi kwa wananchi wakitaka Serikali kurudi kwenye mstari wa udahili kwa kutumia sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma na si vinginevyo.

Mbali na hilo, wabunge wamepaza sauti juu ya suala la uhamisho kwa watumishi wa umma wakihoji inakuwaje baadhi ya wakurugenzi kuzuia au kukwamisha uhamisho wa watumishi kutoka ngazi za juu na kusababisha kero kwa wanandoa.

Kilio cha wabunge juu ya tatizo la ajira na uhamisho, kimekuwa kikiiibuka mara kadhaa bungeni na sasa wameibua kilio hicho wakati wakijadili mapato na makadirio ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2025/26.

Bajeti hiyo imewasilishwa leo Jumatano, Aprili 23, 2025 na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene akiliomba Bunge limpitishie Sh1.354 trilioni.

Kati ya fedha hizo Sh1.17 trilioni matumizi ya kawaida na Sh183.3 bilioni ni fedha za miradi ya maendeleo.

Kilio cha ajira kwa wabunge kilianzia kwenye Hotuba ya Mapato na Matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambako walitaja sababu kubwa ni kujuana kuliko kutazama uwezo wa mtu anayeajiriwa.

Hoja hiyo ilizungumzwa na Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni katika mchango wake kwenye hotuba ya Waziri Mkuu akisema simu za wabunge zimejaa ujumbe (SMS) kwa wanaosaka ajira wakiomba msaada wa kupenyezewa vimemo kwani hakuna namna.

Walichokisema wabunge

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Janejelly Ntate amesema mfumo wa kuajiri umekuwa wa zigizaga na hauleweki kwa kuwa, chombo kilichopewa dhamana nacho kimelala.

Ntate ambaye anatokana na kundi la wafanyakazi, amesema Serikali inatoa ajira kwa sasa kwa kutumia mawakala wengine badala ya kutumia sekretarieti ya ajira ambacho ndicho chombo kinachotambuliwa.

“Sekretarieti ya ajira imekwenda wapi, watu wanatoa ajira kwa utaratibu wa ajabu kabisa, naomba kutolewa mfano wa ajira za hivi karibuni zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yani walitoa tenda kwa NBAA (Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu) kwenye ajira, nani aliwapa mamlaka,” amehoji Ntate.

Pia, amezungumzia alichokita kiburi cha baadhi ya watumishi akihoji kinatoka wapi hata kuwagomea viongozi wa ngazi ya juu kwenye uhamisho au upandishaji wa madaraja.

Ametoa mfano yupo mtumishi alipata uhamisho lakini mmoja wa wakurugenzi wa halmashauri akakataa kumpa kibali bila sababu za msingi licha ya kuwa alikuwa amepokea kutoka wizarani.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Thea Ntara amelalamikia mfumo wa ajira unaotolewa kwa kutumia mawakala akisema unaharibu utaratibu mzima wa kuwapata watumishi.

Dk Ntara anayetokana na kundi la vyuo vikuu ametoa mfano wa ajira za hivi karibuni zilitolewa na TRA kupitia kwa NBAA kwamba haifai badala yake wapewe sekretarieti ya ajira ambayo imejaa wabobezi wengi kwenye taaluma.

Hoja hiyo ikachangiwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Husna Sekiboko ambaye amesema kitendo cha Serikali kutoa majukumu kwa chombo kingine ili kisimanie ajira ni bomu.

Amesema ajira za Tanzania ni mali ya Watanzania na kwamba jambo hilo ni la kiusalama ambalo lazima liangaliwe kwa usalama zaidi lakini kuwapa chombo kingine ambacho hakijui mahitaji ya Serikali ni kosa.

“Mtoto wako unapaswa kumlea wewe na kumlisha, lakini kwenda kumpa mjomba eti amlishe hawezi kushiba, Serikali ina vyombo vingi hebu vitumike kutusaidia kwenye mchujo lakini abadani asipewe mtu mwingine,” amesema Husna.

Amesema chombo kilichopewa dhamana kwa sasa ni kama kimekunja mikono yake na kuweka nyuma huku akisisitiza suala la kuwasaili watu kwenye maeneo yao kwa lengo la kupunguza gharama kwa vijana.

Hoja hiyo ikazungumzwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Alice Kaijage akisema hali siyo nzuri kwenye mfumo wa ajira kwa sababu chombo kilichopewa dhamana hiyo kimejiondoa bila taarifa na haijulikani nani alitoa mamlaka ya kufanya hivyo.

Dk Kaijage amesema katika kipindi cha hivi karibuni alizunguka mikoa mingi na halmashauri kwa ajili ya kuzungumza na watumishi lakini alikutana na vilio ikiwamo uamuzi mwingi wa Serikali kupingwa na watu wa kada za chini.

Mchango wa Mpina

Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ni miongoni mwa waliochangia bajeti hiyo akiuliza utawala bora uko wapi kwa kuwa, ajira za Serikali zinatolewa kama njugu kwa watu ambao hawastahili na kuwaacha wenye sifa na uwezo.

Mpina amesema ziko ajira na teuzi kwenye vyombo vya uamuzi ambao umetolewa kwa wageni wakati wapo raia wa Tanzania wenye sifa na uwezo lakini kwa sababu ya mfumo hawapewi.

“Nasema hayo kwa sababu hivi karibuni tulishuhudia Mkuu wa Majeshi , Jenerali Jacob Mkunda alilisema hili, hadi leo hatujui nani wako kwenye teuzi, nani anashikilia nafasi za uamuzi wakati ni mgeni, sasa hapo utawala bora uko wapi,” amehoji Luhaga.

Mbunge huyo amekosoa ukimya wa Serikali katika ripoti mbalimbali  zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Makuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwamba amekuwa akieleza mambo mengi lakini hakuna ufuatiliaji.

Kingine ametaka Serikali kutoa tamko la kurudisha mihuri ya wenyeviti wa vitongoji walionyang’anywa kwa madai wanauza ardhi lakini akahoji iweje Serikali inawapora hao lakini inashindwa kuwazuia baadhi ya watumishi wanaouza viwanja kimoja kwa watu zaidi ya mmoja.

Hata hivyo, Waziri Simbachawene amesema suala la ajira zilizozungumzwa na wabunge zikiwamo za TRA wamelisikia na hata kama zinafanywa na watu wengine jicho la sekretareti litaangalia lakini, “maoni yenu, ushauri wenu, tumeusikia, tunakwenda kushauriana ndani ya Serikali ili manung’uniko haya yaweze kupungua.”

Januari 22, 2024, katika mkutano wa saba wa CDF na makamanda uliofanyika jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan, CDF Mkunda alisema kuna baadhi ya waomba hifadhi na wakimbizi wameajiriwa na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali serikalini jambo ambalo ni tishio kwa usalama.

Amesema kuwepo kwa muda mrefu kwa waomba hifadhi hao na wakimbizi ni tishio la kiusalama kwa kuwa baadhi yao au familia zao wameajiriwa na wengine kupewa teuzi serikalini katika nafasi zenye kutoa uamuzi.

Rais Samia aliyefungua mkutano huo alisema amechukua angalizo hilo na kuaahidi Serikali kufanya uchambuzi hasa kwa wakimbizi kutoka DRC na kwingineko kuona jinsi ya kuwarudisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *