Tabora. Baada ya wakulima wa zao la tumbaku kudai kwa muda mrefu fedha za mbolea ya ruzuku walizoahidiwa na serikalini bila mafanikio, hatimaye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Stephen Wasira amejitosa katika sakata hilo akisema hadi mwishoni mwa mwezi huu watakuwa wamelipwa.
Wakulima hao wanaidai serikali Sh13 bilioni ilizowaahidi kuwalipa msimu wa mwaka jana na zinazotakiwa kulipwa kwa wakulima hao nchi nzima lakini kati ya hizo asilimia 70 ya fedha watalipwa wakulima wa zao hilo katika mkoa wa Tabora.
Msingi wa madai ya malipo ya fedha hizo kuchelewa ni kitendo cha baadhi ya viongozi ushirika wasiokuwa na nia njema kuongeza idadi ya watu ambao si wakulima kwenye orodha ya watu wanaotakiwa kunufaika na fedha hizo wakati si wakulima wa zao hilo.
Jambo ambalo serikali iligundua na kuamuru mchakato wa uhakiki kuanza upya ambao umechukua muda mrefu sasa ili wabainike wakulima waliolima zao hilo ili waweze kulipwa kiwango chao halali pasina kunufaika na wengine wasio stahili katika fedha hizo.
Baada ya kuelezwa malalamiko hayo, Wasira kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mkoani Tabora, akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa uhai wa chama hicho na utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi wa 2020/2025, alisema anaenda kuongeza msukumo kuona ndani ya mwezi huu wanalipwa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Stephen Wasira akizungumza na kutoa maelekezo kwa wananchi na viongozi mkoani Tabora. Picha na Hawa Kimwaga.
Akizungumza katika mkutano na wananchi pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika mkoa wa Tabora katika viwanja vya TBC Manispaa ya Tabora jana jioni, Wasira alisema fedha hizo zitalipwa.
“Fedha zenu hizi mtalipwa tena mwishoni mwa mwezi huu. Ni lazima tuwasikilize wananchi na tutatue changamoto zao na sisi tulio kwenye nafasi hizi ndio tuna dhamana ya kutatua changamoto zao na tunapozungumzia tumbaku tunazungumzia uchumi ambao pia ni manufaa kwa taifa letu,” amesema Wasira.
Kulingana na Wasira alisema katika ziara hiyo mkoani hapo tatizo kubwa analoulizwa maswali ni kutokulipwa fedha hizo ambalo limejitokeza sehemu nyingi na majibu yake wanayo ni ruzuku ya mbolea.
“Jambo hili nimelikuta Urambo, nimelikuta leo Sikonge, nataka kuwaambia wakulima watumbaku watalipwa ruzuku yao kabla ya mwezi huu kuisha, kilichokuwa kinachelewesha ni uhakiki viongozi wa ushirika walitakiwa waseme mkulima gani ameuza nini nao wakawa wanaongeza watu ambao hawakulima Tumbaku,”alisema Wasira.
Alisema kutokana na changamoto hiyo ilichukua muda mrefu kuhakiki lakini kwa sasa inakamilika na serikali imetenga Sh13 bilioni kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao na kati ya hizo asilimia 70 zitalipwa katika Mkoa wa Tabora.
Baada ya kutoa majibu hayo aliwataka viongozi na watendaji wa nafasi mbali mbali serikalini na ndani ya chama hicho kuongeza kasi ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwani mtaji wa CCM ni watu.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Tabora, Venance Msafiri amesema kwa mkoa huo una jumla ya wakulima 57,000 watanuafaika na fedha hiyo ikiwa sawa na asilimia 70 ya wakulima wote wanaostahili fedha hizo za ruzuku nchini.
Aliongeza kwa kduai elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima ili kuendelea kuimarisha kilimo chenye tija kwa mavuno zaidi.
“wakulima wa Tabora ndio idadi kubwa zaidi kwenye madai ya fedha hizo za ruzuku zilizoahidiwa na Serikali,” amesema
Mkulima wa Tumbaku Mkoa wa Tabora, Adrea Michael amesema kuwa amefarijika zaidi na agizo la Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa la kulipwa fedha zao.
Mrisho Ali ambaye pia ni mkulima wa tumbaku Mkoa wa Tabora, alifurahishwa na msimamo wa Serikali juu ya kukamilisha malipo yao ambayo wameyasubiri kwa muda wa mwaka mzima.
Tumesubiri hizi fedha kwa muda mrefu lakini ni kwa sababu bado tuna imani kubwa na serikali yetu,”amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba ameonya kuwa chama hicho kipo tayari kukabiliana na wapinzani wanaoendesha propaganda ya kuichafua Serikali iliyowekwa na chama hicho.
“Hatuwezi kuwavumilia watu wachache waoichonganisha Serikali na wananchi wake kwa kupeleka maneno ya hovyo majibu tunayo wala hatutasubiri viongozi wa kitaifa waje kuwajibu,” amesema.