Akizungumza jana Jumapili mjini Tehran, na familia za Mashahidi wa Usalama, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya makosa makubwa ya kimahesabu kuhusu Iran na kusisitiza kuwa utawala huo unapaswa kuadhibiwa na kufahamishwa nguvu, irada na ubunifu wa taifa la Iran na vijana wa nchi hii.
Swali muhimu ni kuwa je, ni masuala gani ambayo utawala wa Kizayuni umefanya makosa ya kimahesabu kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran? Kosa muhimu zaidi lililofanywa na utawala huo wa Kizayuni katika uwanja huo ni kupuuza uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuweza kuzuia hujuma ya adui. Kujizuia na subira ya kistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya jinai nyingi zilizofanywa na utawala huo, yakiwemo mauaji ya wanasayansi na makamanda wa kijeshi wa Iran na kushambuliwa baadhi ya maeneo ya Iran, kuliufanya utawala huo unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, ufanye makosa kadhaa makubwa kuhusu nguvu ya Iran ya kuzuia hujuma ya adui.
Kosa la kwanza lililofanywa na utawala huo ghasibu ni kwamba, ulidhani kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kuingia kwenye vita na hivyo haitajibu aina yoyote ya jinai za utawala huo. Kosa la pili ni kwamba ulidhani kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina uwezo wa kuishambulia Israel, hivyo haitajibu jinai nyingi na za mara kwa mara zinazofanywa na utawala huo dhidi yake. Kosa la tatu la kimahesabu la utawala wa Kizayuni ni kwamba kutokana na uungaji mkono mkubwa unaopata kutoka kwa Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kivitendo haitajibu mashambulizi ya kijeshi ya Tel Aviv.

Operesheni za Ahadi ya Kweli ya kwanza na pili na hasa ya pili, zilithibitisha wazi ubatili wa fikra hizo za utawala wa Kizayuni na makosa yake ya kimahesabu kuhusu uwezo wa kuzuia mashambulizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hakika operesheni hizo zilithibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa wa kijeshi sio tu wa kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni, bali hata wa kuchukua hatua kubwa za kijeshi dhidi ya utawala huo, licha ya uungaji mkono mkubwa wa Marekani, na kuwa inaweza kutoa pigo kubwa la kijeshi kwa utawala huo.
Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaza daima kuchukua hatua za kuimarisha nguvu zake za kijeshi. Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei alisisitiza alipoonana siku ya Jumapili na familia za Mashahidi wa Usalama kwamba ni Iran yenye nguvu tu ndiyo inaweza kudhamini usalama na maendeleo ya nchi na taifa. Kwa hivyo, alisema Iran inapaswa kujiimarisha siku baada ya siku katika nyanja zote za kiuchumi, kisayansi, kisiasa, kiulinzi na kiusimamizi.
Jambo jengine muhimu katika makosa makubwa ya kimahesabu yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kuhusiana na Iran ni kuhusu uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa kutilia maanani matatizo ya kiuchumi ambayo yamejitokeza nchini kutokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani na kuwafanya wananchi wapitie maisha magumu, utawala wa Kizayuni ulidhani kuwa uungaji mkono wa wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepungua. Lakini makaribisho na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 na matakwa yao ya kuitaka serikali ikabiliane vilivyo na vitisho na jinai za utawala huo ghasibu ni ishara nyingine ya wazi ya makosa ya kimahesabu yaliypofanywa ma utawala wa Kizayuni kuhusiana na uungaji mkono wa wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuhusiana na suala hili: “Wao wamefanya makosa ya kimahesabu kuhusu Iran kwa sababu hawaijui Iran, vijana na taifa la Iran, na bado hawajaweza kuelewa vizuri nguvu, uwezo, ubunifu na azma ya taifa la Iran, ambapo sisi tunapasa kuwafahamisha Iran ni nini.