Alipoingia madarakani Machi 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan alikuja na maono thabiti kwa Tanzania ya kuhakikisha kila mwananchi anafanya kazi katika mazingira salama. Katika kipindi cha miaka minne, uongozi wake umekuwa wa mageuzi makubwa, ukichanganya uelewa wa changamoto za Taifa na mbinu za kiutendaji.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya utawala wake ni maendeleo makubwa katika usalama na afya kazini, eneo muhimu linaloathiri moja kwa moja ustawi wa Watanzania na uimara wa uchumi.
Kujenga mazingira salama kazini
Tangu mwanzo, Rais Samia alionyesha dhamira thabiti ya kuboresha usalama na afya kazini. Alitambua kuwa nguvu kazi yenye afya si takwimu tu bali ni msingi wa uchumi imara.
Uongozi wake umezingatia ujumuishi, ukihamasisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa. Hii imewezesha Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kutekeleza mipango na sera bunifu ambazo sasa zimekuwa kielelezo cha usalama na afya kazini katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kutekeleza malengo ya mahali salama pa kazi kupitia OSHA
Chini ya uongozi wa Rais Samia, OSHA imebadilika kutoka kuwa chombo cha udhibiti pekee hadi kuwa taasisi shirikishi na yenye ufanisi zaidi.
Mamlaka hiyo imeongeza nguvu za utekelezaji wa kanuni za usalama na afya kazini kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika sekta mbalimbali. Sekta zenye vihatarishi vingi zaidi kama ujenzi, madini na viwanda ambazo kihistoria zilikuwa na viwango vya juu vya ajali, zimeshuhudia kupungua kwa ajali na majeraha kazini.
Hata hivyo, OSHA haikujikita tu katika utekelezaji wa sheria bali pia kuendesha mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi, yakilenga kukuza utamaduni wa usalama na afya na uwajibikaji. Mafunzo haya yamewapa wafanyakazi ujuzi wa kutambua na kupunguza hatari mahali pa kazi, hatua iliyoleta ongezeko la tija na ari kazini, lengo likiwa ni kuwezesha wafanyakazi si tu kuchangia ukuaji wa taasisi zao bali pia kurejea nyumbani wakiwa salama kila siku.
Mkakati wa kuvutia uwekezaji ulivyorahisisha biashara na kukuza usalama na afya
Moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Rais Samia ni utekelezaji wa Mkakati wa kuvutia uwekezaji (Blueprint), ambao umeifanya Tanzania kuwa na mazingira rafiki zaidi kwa biashara na uwekezaji. OSHA imechangia kwa kiasi kikubwa katika mkakati huu.
Katika kutekeleza mkakati huo, OSHA imefuta ada 14 zilizokuwa mzigo kwa wafanyabiashara, ikiwemo ada za usajili wa maeneo ya kazi na ada za leseni za usalama na afya kazini.
Ada hizo zilizofutwa zinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh 37.3 bilioni, kiasi ambacho Serikali imekiacha mikononi mwa wafanyabiashara ili kuwawezesha kuboresha shughuli na mazingira yao ya kazi pamoja na kukuza biashara zao.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (wa tatu kulia), akiendesha shughuli za ukaguzi wa hatua za usalama na afya katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP). Ziara yake ililenga katika kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya usalama na kuhamasisha mazingira salama na yenye afya ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wote.
Zaidi ya hayo, OSHA imerahisisha taratibu za kiutawala. Muda wa kutoa vyeti vya usajili umeshushwa kutoka siku 14 hadi siku moja, huku utoaji wa leseni za uzingatiaji wa sheria na kanuni ukipungua kutoka siku 28 hadi siku tatu pekee.
Kupitia mfumo wa Workplace Inspection Management System (WIMS), OSHA imehamishia usimamizi wa ukaguzi, ripoti za ajali na rekodi za mafunzo ambapo sasa shughuli hizo zinafanyika kidijitali. Mabadiliko haya yameongeza ufanisi na kuwezesha biashara kufuata taratibu kwa uwazi zaidi.
OSHA: Mshirika wa kimkakati katika miradi ya kitaifa
Mbali na majukumu yake ya udhibiti, OSHA imekuwa na mchango mkubwa katika usimamizi wa miradi mikubwa ya kitaifa chini ya utawala wa Rais Samia. Miradi kama vile; Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) na Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) imehakikishiwa viwango madhubuti vya usalama na afya kazini kutokana na usimamizi wa OSHA.
Mamlaka hiyo haikuhusika tu katika ukaguzi bali pia imetoa msaada wa moja kwa moja kuhakikisha hatua za usalama zinazingatiwa katika kila awamu ya miradi hiyo. Mbinu hii ya usimamizi imeimarisha hadhi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa na hivyo kuvutia wawekezaji zaidi.
OSHA na uwezeshaji wa wafanyakazi katika usalama na fursa
Chini ya uongozi wa Rais Samia, OSHA imeongeza uwezo wake wa kuhudumia wafanyakazi kwa kiwango kikubwa. Taasisi hiyo imepata magari zaidi ya 20, imeongeza wafanyakazi wapya 90 na kununua vifaa vya kisasa vya ukaguzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh 6 bilioni.
Rasilimali hizi zimeiwezesha OSHA kufikia maeneo ambayo hapo awali hayakuhudumiwa ipasavyo, hatua iliyoimarisha viwango vya usalama na afya kazini na kupunguza malalamiko ya wafanyakazi.
Mbali na hilo, programu za mafunzo na zana za kisasa za usalama na afya zimewapa wafanyakazi maarifa yanayowawezesha kufanya kazi kwa usalama na afya. Hatua hii imekuwa muhimu katika sekta zisizo rasmi, ambako hatua za usalama na afya zilikuwa duni.
OSHA yaweka alama kimataifa katika usalama na afya kazini
Mafanikio ya Tanzania katika usalama na afya kazini chini ya uongozi wa Rais Samia yameweza kutambuliwa kimataifa. Mipango ya OSHA imeiweka nchi katika nafasi ya mfano wa kuigwa barani Afrika.
Tanzania imefikia hatua nzuri katika kuridhia mikataba muhimu ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu usalama na afya kazini, hatua iliyothibitisha dhamira yake ya kufanikisha viwango vya juu vya usalama. Hatua hizi zimefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, biashara na kuchangia maendeleo endelevu.
Ofisa Mtendaji Mkuu anavyosimamia dhamira ya OSHA
Katika mafanikio haya, kazi ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda ni ya kupongezwa. Uongozi wake umekuwa muhimu katika kuboresha huduma za OSHA kwa kutumia mbinu za kisasa.
Mwenda amesimamia uanzishwaji wa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa taarifa za maeneo ya kazi (WIMS) unaowawezesha waajiri kufuatilia maombi ya leseni kwa njia ya mtandao. Mifumo hii ya kidijitali imefanya taratibu za usajili kuwa rahisi, wazi na rafiki kwa wafanyabiashara.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii walipotembelea kiwanda cha Elewedy Electric na kuthibitisha kama kinatekeleza viwango vya usalama na afya kazini kama ilivyoelekezwa na OSHA.
Pia, amesisitiza elimu kwa umma na utekelezaji wa sheria kwa usawa, akihakikisha OSHA haiishii kusimamia tu viwango vya usalama bali pia kujenga utamaduni wa usalama sehemu za kazi.
Alama aliyoiweka Rais Samia katika usalama kazini
Safari ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan sio tu imebadilisha mtazamo wa Tanzania kuhusu afya na usalama na afya mahali pa kazi lakini pia imeweka msingi imara wa maendeleo ya baadaye.
Uongozi wake, kupitia mipango na mikakati ya OSHA, umejenga urithi wa usalama na afya, tija na ukuaji. Wakati Taifa likiendelea kusonga mbele, mafanikio haya yatabaki kuwa msingi wa simulizi ya maendeleo ya Tanzania, ikitoa mwongozo wa mafanikio katika usalama na afya mahali pa kazi barani Afrika.