Tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tunashuhudia malalamiko ya vilio vya haki, msongamano wa mahabusu, uchelewashaji kesi na ubambikaji wa kesi sasa vyapata muarobaini kwani mama ameipaisha na kuboresha huduma za uendeshaji wa mashtaka ya jinai nchini na kufanya vilio hivyo kuanza kuwa historia!
Nani kama mama? Ni wimbo maarufu wa muziki wa dansi uliotungwa na mwanamuziki nguli Christian Bella na kundi zima la Wana Akudo Sound, tungo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa nchini ikieleza mchango na nafasi ya mwanamke kama mzazi katika jamii.
Na ndivyo yanavyoanza Makala haya maalumu ya kuelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika moja ya duru za sekta ya sheria, uendeshaji wa mashtaka ya jinai, chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Jemedari Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan almaarufu kama “Mama wa Kizimkazi”.
Makala haya yanasawiri kwa mapana na kuelezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita kuanzia mwaka 2021 mwezi Machi hadi Desemba, 2024 kwa kuangazia namna changamoto mbalimbali zilizokua kero kwa muda mrefu kwa wananchi zilivyoweza kupatiwa majibu chini ya Uongozi mahiri na shupavu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai nchini Bw. Sylvester Anthony Mwakitalu.
Taasisi hii ina jukumu nyeti kwa Taifa na kwa wananchi na kwa msingi huo baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani iliweka utashi na uthabiti wa kuleta mageuzi makubwa katika eneo la haki jinai.

Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoani Pwani.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika maboresho ya ofisi ya taifa ya mashtaka
Baada ya kuingia madarakani Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichukua hatua mahsusi ili kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutekeleza majukumu yafuatayo;
Utenganishaji shughuli za mashtaka na upelelezi
Katika kipindi husika (Machi, 2021 hadi Februari, 2025) Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewezeshwa kufungua Ofisi za Mashtaka katika Mikoa yote na Wilaya za makao makuu wa mikoa 26 pamoja na Wilaya 82. Kwa wilaya zilizobaki taratibu zinaendela ili kufungua ofisi katika wilaya hizo. Pamoja na kufikisha huduma hii karibu na wananchi lakini pia imepunguza malalamiko ya kubambikiwa kesi na msongamano wa mahabusi.
Ukaguzi wa magereza na vituo vya Polisi
Katika kipindi miaka minne ya awamu ya sita Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewezeshwa kikamilifu kuweza kukagua magereza na vituo vya polisi kwa lengo la kuainisha changamoto za kiutendaji na kiupelelezi na kutoa maelekezo stahiki kutatua changamoto hizo. Katika kipindi husika, magereza yote yaliweza kutembelewa pamoja na baadhi ya vituo vikubwa vya Polisi. Katika ukaguzi huo, mahabusi 6,465 waliachiwa huru.
Kuongezeka kwa miradi ya ujenzi
Serikali ya awamu ya sita imewezesha kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa Ofisi ambapo mpaka sasa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kutekeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu lilipo Dodoma na ujenzi wa Ofisi katika mikoa 12. Suala hili limeongeza tija katika kazi kwani watumishi wanapata wasaa mzuri wa kufanya kazi na kupunguza gharama za kupanga katika majengo mengine na zaidi usalama wa nyaraka za ofisi.
Kuongeza kwa idadi ya watumishi
Katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita imewezesha kuajili watumishi zaidi ambapo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewezeshwa kuwa na ongezeko kubwa la watumishi wa kada mbalimbali na hivyo kupunguza kwa sehemu changamoto ya upungufu wa rasilimawatu.

Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Ilala.
Kuongezeka kwa bajeti ya mwaka
Bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeongezeka mwaka hadi mwaka ambapo bajeti ya matumizi ya kawaida na maendeleo imeongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/2025.
Kuongezeka kwa vitendea kazi
Maboresho katika ununuzi wa vitendea kazi kama magari, samani na vifaa vingine vya matumizi ya kawaida vimewezesha shughuli za Ofisi kufanyika kirahisi, kuleta hamasa na kurahisisha ufanyaji wa kazi na hivyo kuboresha huduma ya mashtaka kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kuanzisha na kuboresha mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa kesi.
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kuboresha mifumo ya usimamizi wa kesi na kuanzisha mfumo wa TEHAMA wa kusimamia kesi zinazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua mbalimbali. Mfumo huu kwa kifupi unajulikana kama CMIS (Case Management Information System) na mfumo huu umeunganishwa na mifumo mingine ya wadau. umeboresha sana usimamizi wa kesi na kupunguza matumizi ya karatasi ambayo ni gharama.
Kuongezeka kwa kiwango cha kushinda mashauri
Kutokana na kuongezewa bajeti, vitendea kazi, watumishi na mafunzo kumepelekea kiwango cha kushinda kesi kuongezeka ambapo kwa sasa kuna mikakati kabambe ya kuongeza kiwango zaidi ya hapo.
Kupungua kwa mrundiko wa mashauri mahakamani.
Kutokana na miongozo inayotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka katika hatua za upelelezi na uendeshaji mashtaka mahakamani imepelekea mashauri kufunguliwa mahakamani baada ya kupitiwa kwa makini na kuchujwa vizuri ili yale yenye ushahidi pekee kuweza kufunguliwa mahakamani. Hatua hii imepunguza kwa kiasi kikubwa mrundikano wa mashauri yaliyokaa muda mrefu mahakamani (Backlog).
Kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia
Kutokana na kushamiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kushirikiana na wadau wengine imechukua hatua mbalimbali kuratibu upelelezi na kusimamia mashtaka ya mashauri yenye makosa ya ukatili wa kijinsia na hivyo kupunguza kutokea kwa matukio hayo. Hii ni baada ya ongezeko la uwezeshaji ndani ya ofisi hii. Pamoja na hatua zingine umetolewa Mwongozo mahususi wa kushughulikia upelelezi na uendeshaji mashtaka ya makosa ya ukatili wa kijinsia na kuimarishwa kwa dawati la mambo ya jinsia.
Ushiriki wa Msaada wa kisheria kwa wananchi
Katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi chini ya uratibu wa wizara yenye dhamana ya sheria.
Kwa namna ya pekee ushiriki umefanyika kupitia Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa kisheria kwa kuwafikia wananchi wengi haswa wa ngazi cha chini.
Pamoja na hayo chini ya serikali ya awamu ya sita ofisi imeendelea kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya sheria kila mwaka kwa kuweka banda maalumu na kutoa huduma ya msaada wa kisheria.
Kuimarika kwa huduma ya ukaguzi
Katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kuwezeshwa kwa kiasi kikubwa ili kufanya ukaguzi wa huduma za mashtaka katika ofisi za mikoa na wilaya ili kubaini changamoto zilizopo na kuboresha utendaji kazi.
Ni katika kipindi hiki serikali imewekeza sana katika kuwaweka wadau wa haki jinai pamoja na hivyo kufanikisha kazi zinazohitaji ushiriki wa taasisi zaidi ya moja. Katika hili kumekuwa na ukaguzi wa pamoja kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi na TAKUKURU.
Kuanzishwa kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Taasisi za Haki Jinai
Tume ya Rais ya Maboresho ya Taasisi za Haki Jinai kumeleta tija katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwani ni moja ya taasisi ambazo zimependekezwa kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kibajeti, mafunzo na vitendea kazi.
Yapo mapendekezo ya muda mfupi ambayo yameshaanza kufanyia kazi nay ale ya muda wa kati na muda mrefu yatakapofanyiwa kazi yataleta tija zaidi.
Kuboreshwa kwa majukwaa ya Haki Jinai
Katika miaka minne ya serikali ya awamu ya sita majukwaa ya haki jinai yameboreshwa kiuwezo na kibajeti ambapo kwa sasa yanaweza kukutana ngazi ya wilaya na mikoa na kufika taifa ambao hufikisha hoja husika kwa kamati ya mawaziri. Hatua hii imeongeza wigo wa ushirikiano baina ya wadau wa haki jinai na kuboresha huduma ngazi zote za jamii.
Miongozo ya Mkurugenzi wa Mashtaka
Kuwekwa kwa mazingira mazuri yaliyopelekea Mkurugenzi wa Mashtaka kuweza kutoa miongozo mbalimbali ya usimamizi na uendeshaji wa mashtaka mahakamani. Kwa kipindi cha 2021 mpaka Februari 2025 miongozo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka ni pamoja na Miongozo inayohusiana na Ufunguaji mashtaka, Makubaliano ya Kukiri Makosa, Ulinzi wa Mashahidi, mashirikiano ya kimataifa na Utaifishaji Mali.
Miongozo hii imeboresha huduma za mashtaka na kuweka ukomo wa upelelezi kwa yale mashauri ambayo kisheria makosa yake hayana ukomo wa upelelezi na uendeshaji mashtaka. Kwa sasa mashauri yote yamewekewa ukomo wa upelele isipokuwa yale mashauri makubwa na yenye upekee ambayo kibali maalumu kinatolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka kuruhusu ukomo wake kuvuka siku 90.
Changamoto katika utekelezaji wa majukumu
mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yalioainisha hapo juu na mengine ambayo hayajaainishwa ipo changamoto kubwa ya kukosa ushirikiano wa baadhi ya mashahidi katika mashauri na hivyo kupelekea mashauri kukwama kusikilizwa mahakamani.

Jengo la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoani Manyara
Kwa kuangalia mageuzi makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo upatikanana wa huduma za mashtaka hadi katika ngazi za wilaya, ushughulikiaji wa mashauri ya kesi kwa wakati na malalamiko mbalimbali, uratibu wa upelelezi katika viwango vinavyoridhisha na upunguaji wa msongamano wa mahabusu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wamefanikiwa kwa sehemu kubwa kurudisha imani ya wananchi katika vyombo vya upatikanaji wa haki iliyokuwa imeanza kupotea.
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uaminifu. Hata hivyo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inaamini kuwa endapo changamoto hizo zitafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Sita basi kutaongeza tija katika shughuli za uendeshaji mashtaka mahakamani kama ambavyo imetokea katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
HAKI, AMANI NA USALAMA KWA MAENDELEO YA TAIFA