
Dar es Salaam. Januari hii tumetimiza miaka 46 toka alipofariki Mbaraka Mwinshehe, mtunzi, mpiga gitaa la solo na muimbaji mashuhuri, lakini bado jina lake linakumbukwa katika anga za muziki Afrika ya Mashariki.
Mwanzoni mwa mwezi Novemba 2024, niliwakuta vijana wanamuziki wa mtindo wa Singeli wakiwa studio wakirekodi wimbo wa Mbaraka Mwinshehe katika mipigo ya Singeli.
Nadhani angekuwa hai angeshangaa wimbo uliotungwa pengine wazazi wa vijana hawa hawajazaliwa ukirudishwa tena kwenye masikio ya vijana wa zama hizi.
Nyimbo nyingi ambazo Mbaraka alishiriki bado zinasikika hewani zikishindana na nyimbo mpya zinazobuniwa katika zama hizi kwa kutumia teknolojia mpya.
Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro 27 Juni, 1944. Mbaraka alikuwa mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto 12 wa Mzee Mwinshehe Mwaruka aliyekuwa Mluguru msomi, na karani katika mashamba ya katani, na mama yake alikuwa kabila la Kingoni.
Kati ya watoto hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio waliweza kuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia bendi hiyohiyo.
Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Nzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka, Mzee Mwaruka.
Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na kuacha shule ili awe mwanamuziki. Kadri ya maelezo ya mzee mmoja ambaye walikuwa wakisoma pamoja, siku moja Mbaraka kama kawaida yake alikuwa katoroka bwenini kwenda kushiriki dansi, huku nyuma kukafanyika ukaguzi wa waliopo mabwenini, Mbaraka na watoro wenzie wengine wakakosekana, basi kesho yake wote ambao hawakuweko wakatakiwa kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko.
Mbaraka aligoma, akapewa muda akajifikirie, inasemekana alichukua filimbi yake akakaa peke yake akipiga filimbi, hatimaye akaamua kufunga mizigo yake na kuondoka pale shuleni bila hata ya kufukuzwa na waalimu, huo ukawa mwisho wa elimu ya Mbaraka.
Baada ya kuondoka shuleni, Mbaraka aliondoka zake na akapita mbele ya klabu ya wanamuziki wa Morogoro Jazz na kuwakuta wamepumzika nje ya klabu yao, Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha, walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake.
Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi. Wakati huo bendi ilikuwa na shida ya mpiga gitaa la rhythm, hivyo walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali.
Taratibu za bendi hiyo wakati huo ilikuwa ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee waliokuwa wanalipwa mshahara kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi, kwa makubaliano hayo Mbaraka alianza kazi Morogoro Jazz Band.
Siku moja Morogoro Jazz Band ilialikwa Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi mshahara, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, hili likaleta zogo, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa shilingi 150 akagoma kwenda Dar kwa kusisitiza kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo.
Kwenye onyesho hilo, Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Akapandishwa mshahara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana wakati huo, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo mkuu wa Morogoro Jazz Band.
Siku ya Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikisika kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha Mbaraka Mwinshehe, mpiga gitaa muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga kila wilaya ya nchini Tanzania.
Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari.
Kutokana na maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka au maarufu kama Super Zex mwanamuziki mkongwe, siku ya tarehe 12 Januari 1979 alikuwa anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia walitoka kijiji kimoja Maramba huko Tanga.
Anasema alipofika karibu na kanisa la Kongoya aliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar na kwa spidi kali ikaenda na kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.
Ilikuwa mchana kiasi kama saa 7 hivi. Watu wakakimbilia kuangalia ajali akiwemo yeye. Na mara moja akamtambua Mbaraka na kuwaambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe.
Katika gari lile kulikuweko watu watatu Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva. Dereva (maelezo ya baadaye yalimtambua dreva huyo kuwa alikuwa rafiki wa Mbaraka na mkazi wa Moshi aliitwa Omari Abdi, kuna maelezo mengine kuwa Abdi pia alikuja kufia hospitalini si pale kwenye ajali) na abiria aliyekuwa nyuma alikufa palepale, ikalazimika kuanza kukata mabati ili kumuondoa Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile lililoharibika, yeye alikuwa bado hai.
Wakati kazi hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band (Bendi ya Watanzania) ilikuwa ikipiga muziki na kuwaambia kuwa mwenzao kaumia sana, nao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Mbaraka aliweza kutolewa kwenye gari na kupelekwa kwenye hospitali ya Makadara.
Zebedee pia akatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wakipiga Zambia Bar, wanamuziki walipofika hospitali wakaambia watoe damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali.
Muda si mrefu Mbaraka Mwinshehe akafariki akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka alisafirishwa mpaka wa Horohoro na kupokelewa. Mbaraka Mwinshehe alizikwa Nzenga Kisarawe.