
Mwaka 1995, mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China, uliweka historia kwa kupitisha azimio lenye ajenda madhubuti kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia.
Mwongozo uliotokana na mkutano huo, wenye vipengele 12 vya msingi, ulilenga kushughulikia changamoto kama vile umaskini, elimu, afya, uongozi, haki za binadamu, na vyombo vya habari.
Miaka 30 baadaye, ni wakati muafaka wa kutafakari: Tumepiga hatua kiasi gani? Ni wapi tunakosea? Na tunajifunza nini kwa ajili ya mustakabali wa kizazi kijacho?
Takwimu zinaonesha kumekuwa na mafanikio makubwa, hasa katika sekta ya elimu.
Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya wasichana wanaojiunga na elimu ya msingi na sekondari, huku sera ya elimu bila malipo ikiwa mojawapo ya hatua za msingi zilizochochea mafanikio haya.
Kulingana na BEST 2022, asilimia 95 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wameandikishwa. Idadi ya wasichana waliokamilisha elimu ya msingi imeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2000 hadi asilimia 89 mwaka 2022, huku waliokamilisha elimu ya sekondari wakiongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2000 hadi asilimia 72 mwaka 2022.
Katika elimu ya juu, idadi ya wanawake waliojiandikisha katika vyuo vikuu imeongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2000 hadi asilimia 48 mwaka 2022 (TCU 2022), huku wale wa taasisi za ufundi wakiongezeka kutoka asilimia 30 mwaka 2000 hadi asilimia 45 mwaka 2022 (NACTE 2022).
Katika uongozi, wanawake wamepata nafasi zaidi serikalini na sekta mbalimbali, ikiwemo nafasi za juu ya Rais na mawaziri.
Hata hivyo, mwitikio wa wanawake kugombea nafasi za uongozi bado ni mdogo, mwaka 2024 ni asilimia 2.1 pekee ya wanawake waliogombea uongozi wa vijiji na serikali za mitaa (TGNP 2024).
Sekta ya uchumi nayo imeona maendeleo kupitia mifuko ya uwezeshaji wa wanawake, kama asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zinazotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Kumekuwa na ongezeko la wanawake wajasiriamali na zaidi ya asilimia 40 sasa wanamiliki biashara zikiwamo kampuni kubwa kwa mujibu wa takwimu za NACTE 2022.
Aidha, kumekuwa na mabadiliko chanya katika sekta ya afya. Uwekezaji katika vituo vya afya umeimarika, na vifo vya wajawazito na watoto wachanga vimepungua kutokana na huduma bora za afya. Programu za afya ya uzazi zimeimarishwa, huku asilimia 80 ya wanawake wa mijini wakipata huduma za uzazi wa mpango (NBS 2022).
Hata hivyo, licha ya mafanikio haya, changamoto nyingi bado zinadumaza maendeleo ya wanawake.
Mwitikio mdogo wa wanawake katika kugombea nafasi za uongozi ni mojawapo ya masuala yanayojitokeza.
Takwimu kutoka TGNP (2024) zinaonyesha ni asilimia 2.1 pekee ya wanawake waliogombea uongozi wa vijiji na serikali za mitaa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Ukatili wa kijinsia pia bado ni tatizo sugu, huku ndoa za utotoni na ujauzito wa mapema vikichangia wasichana wengi kuacha shule.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) 2022, asilimia 12 ya wasichana wa vijijini bado wanaacha shule kwa sababu ya ndoa za utotoni na ujauzito wa mapema.
Kwa upande mwingine, sekta ya ajira bado inaonyesha ukosefu wa usawa. Wanawake wengi wanajikuta wakilipwa mishahara ya chini licha ya kufanya kazi sawa na wanaume. Takwimu za 2022 zinaonyesha wanawake walilipwa wastani wa asilimia 20 chini ya wanaume katika sekta rasmi (NBS 2022).
Ili kukabiliana na hili, ni dhahiri baadi yetu tungependa kuona mabadiliko ya mtazamo kuhusu usawa wa kijinsia Lazima tukubali kuwa usawa wa kijinsia haumaanishi kumuinua mmoja na kumdhoofisha mwingine.
Tunapaswa kuhakikisha sera na programu zetu zinawawezesha wavulana na wasichana kwa pamoja kwa njia inayohimiza maendeleo ya wote.
Serikali na mashirika ya kiraia, yanapaswa kuhakikisha utekelezaji wa sheria zinazolinda haki za wanawake unafanyika bila kusuasua. Ukatili wa kijinsia hauwezi kuvumiliwa tena na programu za malezi, ushauri na elimu kwa wavulana zinapaswa kuimarishwa ili kuwajengea uwezo wa kushiriki vyema katika jamii. Tunahitaji kubuni mifumo inayowaandaa vijana wa kiume kuwa viongozi na waume bora wa kesho.
Uwekezaji katika wanawake unapaswa kuendana na sera za kuhakikisha kuwa hakuna kundi linaloachwa nyuma. Fursa za ajira, biashara na uwezeshaji wa kiuchumi zinapaswa kuwa shirikishi kwa jinsia zote.