Miaka 25 ya Lady Jaydee na Bongo Fleva

Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongo Fleva, Lady Jaydee, 45, mwaka huu unaadhimisha miaka 25 tangu ametoka kimuziki na sasa anaheshimika na wengi kama msanii aliyeweza kuwa katika kilele cha mafanikio ya kazi yake kwa muda mrefu zaidi. 

Kwa kipindi hicho amekuza jina lake kama chapa yenye ushawishi katika tasnia ndani na nje, ameshiriki katika miradi ya kijamii hasa inayowahusu wanawake na watoto huku akipigana na kushinda vita vingi vya kibiashara vilivyomkabili. 

                    

Nyimbo zake zimekuwa maarufu kabla ya ujio wa mitandao ya kijamii kama Instagram, YouTube na TikTok ambayo wasanii wengi wa sasa wanaitumia sana kutangaza kazi zao na kuifanya kama kipimo cha kujua namna gani wanakubalika. 

Kwa mujibu wa Lady Jaydee kabla ya muziki, alifanya kazi ya hoteli huko Zanzibar, kisha kusomea Uandishi wa Habari katika Chuo cha Times School of Journalism (TSJ), na mmoja wa walimu wake ni Ayub Rioba ambaye sasa ni Mkurugenzi wa TBC. 

Mambo yalibadilika baada ya kushinda shindano la DJ Show ya Radio One, hivyo kuzawadiwa nafasi ya kufanya kazi na MJ Records ambapo alirekodi wimbo ‘Sema Unachotaka’ ulioweka kwenye albamu, Asubuhi (2000) iliyokuwa na nyimbo za wasanii wengine. 

                  

Albamu yake ya kwanza, Machozi (2001) yote ilirekodiwa MJ Records kwa Master J, kisha zilifuata nyingine kama Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013), Woman (2017) na 20 (2021). 

Miaka miwili iliyopita alitoa albamu ya ushirikiano akiwa na Rama Madee, Love Sentence (2023) yenye nyimbo 10 ikiwa ni albamu ya tisa kwa Lady Jaydee na kumfanya kuendelea kushikilia rekodi kama msanii wa kike wa Bongo Fleva mwenye albamu nyingi. 

Kwa ujumla Jide ni wa pili baada ya Sugu (10), kisha anafuatiwa na Nikki Mbishi (8), Soggy Doggy (5), Juma Nature (5) Harmonize (5), Professor Jay (4), Mh. Temba (3), Fid Q (3), Diamond Platnumz (3), Alikiba (3), Barnaba (3), Navy Kenzo (3). 

Ila tangu mwaka 2010 Nikki Mbishi ndiye msanii aliyetoa albamu nyingi zaidi; Sauti ya Jogoo (2011), Malcom XI (2013), Ufunuo wa Unju Bin Unuq (2015), Sam Magoli (2018), Welcome to Gamboshi (2022), K.I.G.U (2024), Katiba Mpya (2024) na Spana za Unju (2024).
Mapokezi mazuri na mafanikio makubwa ya nyimbo zake tamu za kubembeleza, kuhamasisha na hata alizotumia kutemea nyongo kwa aliopishana naye, yalimfanya Lady Jaydee kushinda na kutunukiwa tuzo zaidi ya 35 kwa miaka 15 mfululizo. 

Tangu mwaka 2000, aliposhinda tuzo ya Clouds FM kama Mwimbaji Bora wa Kike, Lady Jaydee alikuwa akishinda kila mwaka hadi 2015, aliposhinda tuzo za Watu kama Mwanamuziki wa Kike Anayependwa. 

Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), zilizoanzishwa mwaka 1999, Jide ameshinda tuzo takribani 14 akiwa ni msanii wa tatu aliyeshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote akiwa ametanguliwa na Diamond Platnumz aliyeshinda 22 huku Alikiba akiwa na 18. 

                      

Ukiachana na TMA, ameshinda tuzo nyingine kama Pearl of Africa (5), Channel O (3), Tanzania People’s Choice (2), Kisima (2), Clouds FM (2), M-Nets Africa, Tanzania Youth, BBC, Uganda Divas, AFRIMMA, Baab Kubwa Magazine, Kenya Bingwa, EATV.

Jide ameshirikiana na wasanii wengi ila muungano wake na Mwana FA ulikuwa moto sana, baadhi ya nyimbo walizoshirikiana ni kama Sitoamka (2002), Wanaume kama Mabinti (2003), Alikufa kwa Ngoma (2004), Hawajui (2005) na Msiache Kuongea (2009).  

Mwana FA ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pia yeye na Lady Jaydee walishirikishwa na Ngwea katika wimbo wake ‘Sikiliza’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, A.K.A Mimi (2004) chini ya Bongo Records.  

Alifanikiwa kushirikiana na Oliver Mtukudzi kutoka Zimbabwe katika wimbo wake, Mimi ni Mimi (2011) baada ya mkali huyo wa Afro Jazz kuja nchini kutumbuiza ambapo Jide alipata nafasi ya kuimba naye jukwaani wimbo wake maarufu, Neria (1991).

Wasanii wa kimataifa waliomvutia ni pamoja na Whitney Houston, Dr. Dre na baadaye sana Rihanna ambaye kwa mujibu wa Lady Jaydee, melodi zake ndizo hasa zilifanya kumkubali baada ya kizazi cha kina Whitney kupita. 

Novemba 2022, kupitia onyesho lake la ‘Suluhu Concert’ alizindua mfuko wake wa hisani, Binti Foundation wenye lengo la kuwainua wanawake huku uzinduzi huo ukiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye. 

Huyu ni wasanii wa mwanzo kuanza biashara ya vyakula na vinywaji kupitia chapa yake ya Nyumbani Lounge, kisha wakafuata mastaa wengine kama Shilole (Shishi Food), Esha Buheti (House of Food), Lamar (Fishcrab Food), Isha Mashauzi (Tamtam Food Point). 

Kulingana na ujumbe wa Lady Jaydee aliouchapisha X, zamani Twitter hapo Desemba 2023, aliwataja Sugu na  Professor Jay kama watu ambao hawakumuacha wakati wa mgogoro wake na mdau mmoja na chombo cha habari alichokuwa akikisimamia. 

“Ni Professor Jay na Sugu, wasanii ambao wamewahi kusimama na mimi katika kutengwa kwangu. Watabaki kwenye historia yangu milele,” aliandika Jide ambaye amemshirikisha Professor Jay katika wimbo wake, Joto Hasira (2013). 

Alirejea tena ujumbe kama huo Oktoba 2024 baada ya kutumbuiza katika Bongo Flava Honors, alichapisha picha akiwa na Sugu na Professor Jay katika onyesho hilo na kusema hao ni ndugu zake sasa na si marafiki tena.