Marekani. Baada ya uchunguzi uliofanywa kwa takribani wiki tatu, hatimaye rapa na mwanamitindo, A$AP Rocky ameachiwa huru kufuatia mahakama kumkuta hana hatia kwenye tuhuma mbili zilizokuwa zikimkabili, ambazo ni kumshambulia kwa kutumia bunduki rafiki yake wa zamani kutoka ASAP Mob, ‘Asap Relli’ mwaka 2021, pili ni kumtishia uhai
Katika chumba cha mahakama baada ya hakimu kutoa kauli kuwa, rapa huyo hana hatia, A$AP alimkimbilia Rihanna ambaye ni mama watoto wake kisha kukumbatiana.

Baada ya kutoka nje ya chumba cha mahakama Rihanna alisikika akisema “Oh Mungu wangu” huku akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake.
Mama mzazi wa A$AP pia alikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria kwenye kesi hiyo naye alitoa shukurani kwa kila mtu aliyeonesha kumsaidia kijana wake.
Naye A$AP alipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka nje ya chumba cha mahakama na kuweka wazi hisia zake za furaha, baada ya kushinda kesi hiyo iliyomgharimu muda wa miaka minne.
“Tukio hili lote limekuwa kama wazimu miaka hii minne iliyopita. Lakini ninashukuru, na nimebarikiwa kuwa hapa sasa hivi. Kuwa mtu huru kuzungumza na wewe,” amesema Asap.

Mshtaki wa ASAP Rocky ambaye ni rafiki yake wa zamani ASAP Relli, alitoa ushahidi kuhusu kesi hiyo Januari 28, 2025 akielezea mashtaka mawili ya unyanyasaji aliyofanyiwa na rapa huyo Novemba 6, 2021 katika mtaa wa Hollywood Los Angeles, California nchini Marekani akisema kuwa ASAP Rocky alimnyooshea bunduki akitaka kumuua.
Kutokana na sheria za mahakama hiyo ya Marekani na uzito wa kesi zilizokuwa zikimkabili iwapo angepatikana na hatia rapa huyo wa New York ‘ASAP Rocky’ ambaye jina lake halisi ni Rakim Mayers, angefungwa jela miaka 24.