Mhandisi wa program za kompyuta wa Iran, Alireza Zakeri ametangaza kujiuzulu kutoka shirika la Google kutokana na ushirikiano wa kampuni hiyo kubwa ya kiteknolojia ya Marekani na utawala katili wa Israel katika mauaji ya kimbari ya utawala huyo dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Tokea Oktoba mwaka jana Google imekuwa ikishirikiana na Israel katika operesheni za kijeshi ambazo zimepelekea zaidi ya Wapalestina 44,000 kuuawa shahidi, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
Katika chapisho kwenye akaunti yake la Linkedin siku ya Jumatatu, Zakeri ameandika: “Nina furaha kutangaza kwamba nimejiuzulu kama mfanyakazi wa Google! “uamuzi huu unaonyesha maadili yangu.”
Ameongeza kuwa: “Baada ya kupata taarifa kuhusu ushiriki wa Google katika Mradi wa Nimbus, nilielezea wasiwasi wangu kwa miezi kadhaa. Kwa bahati mbaya, licha ya juhudi za wafanyakazi wengi, uongozi ulichagua kudumisha msimamo wake na kutupilia mbali wasiwasi wetu wa pamoja.”
Mradi wa Nimbus ni mkataba wa dola bilioni 1.2 kati ya utawala wa Israel na Amazon na Google. Lengo la mradi huu ni kutoa taarifa za kijasusi kupitia Akili Mnemba (Artificial Intelligence) na kadhalika ambazo hutumiwa na jeshi la Israel kutekeleza mauaji ya kimbari Gaza.

Zakeri amesema: “Kuishi kwa njia ambayo inakinzana na maadili yako ya msingi ni changamoto kubwa. Kuchagua kuondoka hakukuwa rahisi, lakini ilikuwa ni lazima. Kwa kila anayekabiliwa na hali kama hii, natumai utapata ujasiri wa kutanguliza kanuni zako.” Zakeri amehoji: “Kuna faidi gani kuupata ulimwengu wote kisha kukosa dhamiri?”
Mnamo Mei 14, mamia ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina na walio dhidi ya utawala katili wa Israel waliandamana kupinga uhusiano wa Google na jeshi katili la Israel katika mkutano wa kila mwaka wa kampuni hiyo ya teknolojia huko Mountain View.
Waandamanaji walijifunga kwa minyororo karibu na lango la mkutano kulalamikia uhusiano huo.