Mgunda: Msihofu, Namungo haishuki

WAKATI Namungo inapambana kujiengua kwenye hatari ya kushuka daraja, Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema anafahamu mtihani alionao, lakini akiwatoa hofu mashabiki kuwa wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki licha ya ugumu walionao.

Kocha huyo aliyetua Namungo akichukua mikoba ya Mwinyi Zahera, ameiongoza Namungo kwenye mechi 16, ameshinda nne, sare tano na vipigo saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema anafahamu ugumu utakavyokuwa kwenye mechi zilizobaki akiamini wachezaji wanatambua ukubwa wa Namungo na mikakati waliyo nayo kwani yeye ni muumini wa nidhamu.

“Ni kweli mtihani upo, lakini changamoto haikimbiwi bali ni kuitumia fursa. Nimeongea sana na wachezaji naamini kuhakikisha tunakuwa bora kwenye mechi saba zilizobaki ambazo tunakutana na timu zote ambazo pia zinahitaji matokeo mazuri kama sisi, lakini naamini tutafanya vizuri,” alisema Mgunda.

Timu hiyo ambayo ipo Dodoma kwa ajili ya maandalizi jana Jumamosi Machi 29 ilishuka kujipima nguvu na Dodoma Jiji na kuambulia kipigo cha mabao 3-0, Mgunda alisema licha ya kuambulia kipigo wachezaji wake walicheza mpira mzuri na anaamini makosa waliyoyafanya atayafanyia kazi kabla ya kusafiri kuifuata Pamba Jiji kwa ajili ya mchezo wa ligi.

“Ni kweli hatujapata matokeo mazuri dhidi ya Dodoma Jiji kwenye mchezo wa kirafiki kujiweka fiti tayari kwa kuikabili Pamba Jiji, lakini nimefurahishwa na namna wachezaji wangu walivyojituma nimegundua mapungufu machache nayafanyia kazi kabla ya kuikabili Pamba Jiji,” alisema.

“Ligi inaelekea ukingoni mambo ni magumu bila mipango thabiti unapoteza kila kitu. Hicho tumekiona mapema hatutarajii kufanya makosa.” Namungo itakuwa ugenini Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana wakiwa kifua mbele baada ya kuambulia pointi tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani wakishinda bao 1-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *