Mgunda ala kiapo Namungo, ajipa matumaini mechi saba

KOCHA Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda amesema hana wasiwasi na kikosi chake kwenye vita ya kubaki Ligi Kuu Bara kwani amefanya maandalizi ya kutosha yatakayowawezesha kuvuna alama za kutosha na kuepuka vita ya kushuka daraja.

Namungo FC itakuwa ugenini kesho kuanzia saa 8:00 mchana kuikabili Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara raundi ya 24 utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Timu hiyo inakamata nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo 23, ikishinda sita, sare tano na kupoteza 12, huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 28 na kukusanya alama 23.

Tangu aanze kazi klabuni hapo Oktoba 20, 2024, Mgunda ameiongoza Namungo katika mechi 14, na kushinda tatu, sare tano na kupoteza nane huku akivuna alama 14.

Matokeo ya Namungo chini ya Mgunda, KMC (1-0), Mashujaa (1-0), Yanga (2-0), Kagera Sugar (1-1), Ken Gold (2-3), JKT Tanzania (0-0), Fountain Gate (1-2), Tabora United (2-1), Dodoma Jiji (2-2), Tanzania Prisons (0-1), Simba (3-0), Coastal Union (0-0), Azam FC (1-1) na Singida Black Stars (1-0).

Akizungumza leo, Aprili Mosi, 2025 jijini Mwanza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mchezo wa kesho dhidi ya Pamba Jiji, Mgunda amesema wametumia vyema muda wa kupisha mechi za timu ya taifa kufanya maandalizi ya kutosha yatakayowawezesha kubaki kwenye michuano ya Ligi Kuu.

“Hizi wiki mbili za mapumziko tumezitumia vizuri kuboresha kikosi chetu na tunaamini tuko tayari kucheza kwa mchezo wa kesho na kutimiza malengo ya klabu yetu. Maandalizi ya kuendelea na ligi yetu wana Ruangwa wanatambua hilo na wanaelewa kabisa hiki ninachokisema na wanayatambua vizuri maandalizi tuliyoyafanya,” amesema Mgunda.

Kuhusu mchezo wa kesho, Mgunda amesema wanatambua utakuwa mgumu kutokana na timu zote mbili kuhitaji ushindi ili kupanda nafasi za juu, huku akiwahakikishia mashabiki wa timu hiyo kwamba wamejiandaa vya kutosha kuwapa furaha.

“Mpaka tumefika Mwanza ina maana utayari wa kucheza mchezo wa kesho upo, Pamba wana mwalimu ambaye tumecheza pamoja akiwa Yanga Mimi niko Coastal Union kwahiyo tunafahamiana hivyo kutakuwa na ushindani kwa kuwa tunalielewa hilo na kulitambua maandalizi ya kucheza mchezo huo yamekamilika na tuko tayari,” amesema Mgunda.

Mchezaji wa Namungo, Erick Kapaito amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wana motisha ya kutosha kucheza mchezo wa kesho kwani mechi saba zilizobaki ni muhimu kwao.

“Kama timu hata mazoezini kila mmoja anapambana kuhakikisha benchi la ufundi linaridhika na makocha wetu wanatupa maelekezo kuhakikisha tuko kamili naamini kesho tutaonyesha hicho. Tuwaahidi mashabiki wetu kuwa tumekuja kukusanya alama tatu naamini tunastahili hilo, hivyo, watuombee ili tufanikishe hilo,” amesema Kapaito.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *