
MASHABIKI wa soka nchini wanahesabu saa tu kwa sasa kabla ya Yanga na Simba kushuka uwanjani kesho Jumamosi katika pambano la duru la pili la Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hilo ni pambano la 114 kwa timu hizo katika ligi hiyo na kama zilivyo kwa dabi zote, limeanza kuwapa presha mashabiki wao, huku wadau mbalimbali nao wakilijadili kutokana na aina ya vikosi vinavyoenda kukutana kesho na hasa mbio za ubingwa zilivyo kwa timu hizo.
Baadhi ya nyota wa zamani wa timu hizo na makocha wa timu mbalimbali wamezifuatilia timu hizo na hapa ni mitazamo na maoni yao kabla ya watani wa jadi hao hawajashuka uwanjani kuonyeshana kazi kuanzia saa 1:15 usiku. Nahodha na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyekuwa na kismati cha kuitungua Yanga enzi akikutana nao katika Dabi iwe ye Ligi Kuu au ya michuano mingine, amesema mnyama ana kila sababu ya kupata ushindi kwenye mchezo huo akitaja sababu tatu.
“Ni mechi ngumu kutokana na ubora wa vikosi vyote, kuanzia kwenye viwango vya timu mbili zinazowania ubingwa lakini kwangu naiona Simba ikichukua alama tatu haijalishi matokeo ya nyuma yalikuwaje,” alisema na kuongeza kocha huyo msaidizi wa Simba Queens na kuongeza;
“Simba inahitaji pointi tatu ili kukimbizana na mbio za ubingwa hivyo hivyo kwa Yanga ni dabi ya mvuto sana na siku zote nasema mafahari wawili wanapokutana haujawahi kuwa mchezo rahisi.
“Safari hii wanakutana wakati ambao Simba imejipata karibu kila eneo, safu ya ushambuliaji ni bora anaeanza Ateba hapishani sana na Mukwala hivyo inampa wakati mzuri kocha nani wa kuchagua kuanza nae kwa wakati gani.”
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema alisema dabi hiyo haitabiriki na yeye anatoa asilimia 50/50 akiamini kila timu ina uwezo wa kuondoka na pointi tatu.
“Nafikiri mechi hizo hazitabiriki huwezi kwenda na rekodi zilizopita kwa sababu ni mechi kubwa zinaangaliwa na watu wengi kutokana na ukubwa wao Tanzania na Afrika,” alisema Mourinho na kuongeza
“Ukiangalia vikosi vyote vinaendana kuanzia ubora wa ligi lakini kidogo Yanga ina faida kwa sababu wachezaji wake ni wazoefu tofauti na Simba ambayo bado inajenga timu wakati huohuo inakimbizana na mbio za ubingwa.
Timu hizo zinakutana huku, Yanga ikiwa wenyeji wa mchezo baada ya mechi ya awali iliyopigwa Oktoba 19 mwaka jana, kushinda bao 1-0 la kujifunga la beki Kelvin Kijili, huku Simba ikiwa na deni la kuondoa unyonge wa kupoteza mechi nne mfululizo zilizopita mbele ya watani wao hao.
Yanga ambao ni watetezi wa Ligi ndio wanoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 58, nne zaidi na ilizonazo Simba inayoshika nafasi ya pili, ikiwa pia na mechi moja mkononi, kwani Yanga imecheza 22 wakati Wekundu wa Msimbazi wamecheza 21 hadi sasa.