Mgogoro wa hali ya hewa wachukua nafasi kubwa katika mkutano wa G20 nchini Brazil

Migogoro ya hali ya hewa na vita nchini Ukraine na Mashariki ya Kati ilichukua nafasi kubwa katika siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa G20 nchini Brazil jana Jumatatu.

Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi wa kundi la mataifa makubwa ya kiuchumi duniani wameangazia mateso ya watu huko Ukanda wa Gaza na Ukraine, na kutoa wito wa ushirikiano katika kupunguza umaskini, sera ya kodi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Simon Stiell, Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, siku ya Jumamosi aliwasihi viongozi wa G20 kusaidia kuondoa mkwamo katika mazungumzo ya ufadhili wa hali ya hewa katika mazungumzo ya COP29 nchini Azerbaijan.

Mkutano wa kilele wa hali ya hewa unalenga kufikia makubaliano ya kukusanya mamia ya mabilioni ya dola katika kukabiliana na hali ya hewa na ufadhili wa kukabiliana na hali hiyo kwa nchi zinazoendelea.

Ni nchi kubwa za viwanda na ambazo zinahusika na zaidi ya robo tatu ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, ndizo zinadhibiti mikoba ya kiuchumi duniani.

Taarifa ya G20 imetoa wito wa “kuongezwa haraka na kwa kiasi kikubwa ufadhili wa hali ya hewa kutoka mabilioni hadi matrilioni ya dola kutoka vyanzo vyote.

Pamoja na hayo wapatanishi wa COP hawakukubaliana kuhusu kiwango che fedha zinazopaswa kulipwa na mataifa tajiri kuhusiana na suala hilo.

Nchi zilizoendelea zimesema kuwa msingi wa wachangiaji unahitaji kupanuliwa ili kujumuisha mataifa tajiri yanayoendelea kama vile China na nchi tajiri za Mashariki ya Kati.

Mapema leo Jumanne, viongozi wa G20 wanatarajiwa kujadili maendeleo endelevu na ya mpito kuhusu nishati safi.

Wanataka kuongeza juhudi za kupambana na ongezeko la joto duniani kabla ya Donald Trump kuingia rasmi madarakani nchini Marekani.

Trump ametishia kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa hali ya hewa wa Paris na kutoiwajibisha Washington kuhusiana na suala hilo.