Kimsingi kila mwaka baraza hilo linaloshughulikia masuala ya wakimbi la Norway ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, huorodhesha migogoro 10 iliyopuuzwa zaidi duniani.
Kuna vigezo vitatu vinavyozingatiwa na shirika hilo kabla ya kuorodhesha migogoro hiyo. Kwanza ni ukosefu wa ufadhili wa shughuli za misaada ya kibinadamu, kushindwa kwa vyombo vya habari kuangazia migogoro hiyo na tatu ni kutojishughulisha kisiasa kwa jumuiya ya kimataifa.Cameroon imeshaandamwa na migogoro ya kibinadamu mara tatu katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Nchi hiyo imeshuhudia mgogoro wa muda mrefu wa mapambano kati ya makundi yenye silaha katika eneo la msitu linalozunguuka ziwa Chad,imewahi pia kushuhudia machafuko makubwa kwenye maeneo yake ya kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi ambako kunakaliwa na jamii kubwa ya walio wachache ya wanaozungumza lugha ya Kiingereza,na kuendeleza ukosefu wa Utulivu kwenye eneo hilo.
Shirika la NRC linasema kufikia mwaka 2024 kiasi watu milioni 3.4 walikuwa katika hali ngumu ya maisha wakihitaji msaada wa dharura na ulinzi.
Na zaidi ya watu milioni 1.1 walikuwa wameachwa bila makaazi ndani ya nchi hiyo huku kiasi nusu ya wakimbizi na waomba hifadhi waliokimbilia usalama kwenye nchi hiyo walibakia katika njia panda ya kutoelewa hatma yao ya kupata msaada.
Ripoti ya shirika hilo imekwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba licha ya kushuhudiwa hali mbaya ya kibinadamu vyombo vya habari viliipuuza na kushindwa kuripoti huku jumuiya ya Kimataifa nayo ikijiweka kando kabisa wakati fedha zilizotolewa kusaidia kufadhili msaada wa kibinadamu zikiwa ni asilimia 45 tu ya kiasi kilichotakiwa.
Mataifa mengine yenye migogoro ya kibinadamu iliyopuuzwa
Na kwahivyo shirika la NRC linasema mgogoro wa Cameroon ni kisa kimoja cha migogoro ya kibinadamu iliyopuuzwa duniani ,na kutoripotiwa lakini pia kutopata msaada wa ufadhili wa kifedha.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo ikiwa hatua hazitochukuliwa basi hana shaka hali itakuwa mbaya zaidi katika mwaka huu 2025 kwa mgogoro huo.Kadhalika limebaini kwamba kati ya migogoro 10 ya kibinadamu iliyopuuzwa duniani 8 iko barani Afrika.
Mataifa mengine yenye migogoro ya kibinadamu iliyopuuzwa ni pamoja na Ethiopia, Msumbiji, BurkinaFaso, Mali, Uganda, Iran, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Honduras na Somalia.
Katika mwaka 2024 shirika hilo linasema chini ya nusu ya ufadhili ndio uliotolewa kusimamia migogoro hiyo wakati ulimwengu ukitumia fedha nyingine kufadhili bajeti za ulinzi.
Ufadhili mdogo kwa mashirika ya kibinadamu
Katibu mkuu wa NRC amesema ni masikitiko kuona kwamnba mshikamano wa kilimwengu unafunikwa na sera za misingi ya siasa za kizalendo katika mataifa ambayo yaliwahi wakati mmoja kuwa mataifa yanayotowa kwa wingi msaada.
Katika bara la Ulaya, Marekani na kwengineko hali inayoonekana kwa sasa ni mataifa mengi kuitupa mkono sera ya ufadhili na kuwapa mgogo raia kipindi ambacho wanahitaji kusaidiwa.