Mfungaji bora Ligi Kuu kupatikana hivi

Dar es Salaam. Nyota watatu wanaoongoza chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu kila mmoja akiwa amepachika mabao 10 ambapo wawili kati yao ni wa timu moja.

Wachezaji hao ni washambuliaji Clement Mzize na Prince Dube wa Yanga na mwingine ambaye amfumania nyavu mara 10 ni kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua.

Zikiwa zimebaki raundi 10 kwa timu zao kumaliza Ligi Kuu msimu huu, hapana shaka ndoto ya kila mmoja kati ya hao watatu na hata wengine walio chini yao kwenye chati ya kufumania nyavu ni kumaliza msimu akiwa mfungaji bora wa ligi hiyo.

Mchezaji atakayefunga idadi kubwa zaidi ya mabao kuliko wengine ndiye ataibuka mshindi wa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu lakini ikitokea wachezaji wawili au watatu wamelingana idadi ya mabao na wote ndio wamefunga idadi kubwa ya mabao, mshindi atakuwa ni mmoja tu na sio wawili kama ilivyofanyika katika msimu wa 2022/2023 na msimu wa 2023/2024.

Kanuni ya 11 ya Ligi Kuu msimu huu imefafanua vigezo ambavyo vitatumika kuamua mshindi wa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu iwapo wachezaji wawili au zaidi watalingana kwa idadi ya mabao ya kufunga.                                                   

“(13) Mshindi wa tuzo ya Mfungaji Bora ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kuliko wengine katika shindano husika. Ikitokea wachezaji zaidi ya mmoja wamefungana idadi ya mabao, vigezo vifuatavyo vitatumika kwa kufuata mpangilio ili kumpata mshindi;

“13.1 Magoli yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na alama mbili (2) na magoli yaliyofungwa kwa njia ya penati yatakuwa na alama moja. (1). Mchezaji mwenye alama nyingi atakuwa mshindi.13.2 Endapo watalingana alama, mchezaji aliyecheza muda mchache zaidi atakuwa mshindi.

“13.3 Endapo watafanana katika vigezo vyote viwili hapo juu, mchezaji aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi. 13.4 Katika mashindano ya mtoano, Mshindi atakuwa mchezaji ambaye timu yake imefika hatua ya juu zaidi kuliko mwingine na endapo hatua hii haitatoa mshindi kipengele cha i-iii vitatumika kwa mpangilio wake,” imefafanunua kanuni hiyo.

Ikitokea hali ya sasa ikaenda hadi mwisho mambo yanaweza kuwa mazuri kwa Clement Mzize kwani hana goli la mkwaju wa penalti na amecheza kwa muda mchache zaidi kulinganisha na Dube na Ahoua.

Dube naye hana bao la penalti hadi sasa lakini yeye amecheza kwa dakika nyingi kwenye kikosi cha Yanga kuliko Mzize.

Mechi tisa tu ambazo zinaweza kuwa za kujitetea kwa Dube na Mzize ni dhidi ya timu za Pamba Jiji, Coastal Union, Simba, Azam, Tabora United, Dodoma Jiji, Namungo FC, Fountain Gate, na Tanzania Prisons.

Simba imebakisha mechi 10 ambazo zinaweza kumfanya Ahoua amalize akiwa kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu msimu huu ambazo ni dhidi ya Coastal Union, Yanga, Singida Black Stars, Dodoma Jiji, KenGold, Pamba Jiji, JKT Tanzania, Kagera Sugar, Mashujaa na KMC.