Mfumo wa ununuzi uliyookoa mamilioni ya fedha Tanzania

Dar es Salaam. Tanzania imefanikiwa kuokoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 4.95 kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), ambao umepunguza matumizi ya karatasi.

Mafanikio haya yamechangia mfumo huu wa kisasa kuingia miongoni mwa mifumo mitano bora barani Afrika katika Mashindano ya Tuzo ya Ubunifu wa Mifumo yanayoendelea jijini Kampala, Uganda, chini ya uratibu wa Chama cha Afrika cha Utawala wa Umma (AAPAM) kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU).

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, wakati akielezea kuhusu mfumo huo mbele ya jopo la majaji wa kitaalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika jana Novemba 25, 2024.

Simba alibainisha kuwa mfumo wa NeST, uliobuniwa na wataalam wa Tanzania, umekuwa suluhisho muhimu kwa changamoto zilizokuwepo katika ununuzi wa umma.

“Hadi Oktoba 2024, zaidi ya wazabuni 25,000 wamejisajili kwenye mfumo huu, huku Mashirika ya Ununuzi zaidi ya 30,000 yakitumia NeST kuboresha michakato yao. Watumiaji waliosajiliwa wameunda akaunti 41,300, na programu ya NeST kwa simu imepakuliwa na zaidi ya watu 30,000, ikiwa na alama ya nyota 4.3 kwa urahisi wa matumizi,” alisema.

Simba yuko Uganda pamoja na Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA wa PPRA, Michael Moshiro, na Mtaalam wa Ununuzi, Dk. Magoti Harun.

Mafanikio haya yanatokana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyetoa wito kwa Serikali kutumia teknolojia kutatua changamoto za ununuzi wa umma.

Fainali za mashindano hayo zitafanyika Novemba 28, 2024, jijini Kampala, ambapo mshindi atatangazwa mbele ya wadau mbalimbali wa sekta ya ununuzi wa umma kutoka barani Afrika.

Jopo la majaji limefanya tathmini ya kina kabla ya kufikia hatua ya usaili wa uwasilishaji.