Mfumo wa malipo waliza watumishi wa umma, wawakilishi waingilia kati

Unguja. Licha ya Serikali kuanzisha Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Utumishi na mishahara ili kuboresha utendaji na kupata takwimu sahihi za wanaolipwa mishahara, umetajwa kukabiliwa na changamoto huku ukiwalipa watumishi wa umma mishahara pungufu na kuzua taharuki.

Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali kuangalia namna ya kufanya marekebisho na kuubadilisha.

Wamesema kitendo cha kuwapatia watumishi mishahara pungufu kinawaondolea morali ya kufanya kazi na utulivu kwa watumishi hao.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Mei 7, 2025 wakati wa kkutano wa 19 wa Baraza la wawakilishi unaoendelea mjini Unguja.

Mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali amesema kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, watumishi wanapata mishahara tofauti na uhalisia wao, wengine wakipata robo ya mshahara kutokana na mfumo huo ambao umeanza kutumika rasmi Februari mwaka huu.

Mwakilishi huyo amesema licha ya Serikali kuanzisha mifumo hiyo ili kubaini wanaolipwa mishahara hewa, lakini wapo watumishi wanaoendelea kupokea mishahara hiyo tena wakiwa nje ya Zanzibar.

“Hili halipo sawa, watumishi sasa ni zaidi ya miezi mitatu wanaingiziwa mishahara kidogo kwa sababu ya makosa ya kimfumo, ni lini sasa litakwisha na watumishi kuwaondolea wasiwasi huu,” amehoji.

Mwakilishi wa Wawi, Bakari Hamad Bakari amesema kumekuwapo na ucheleweshaji wa taarifa kutoka taasisi moja kwenda nyingine, hivyo kusababisha ucheleweshaji wa kufanyiwa kazi na maendeleo.

Katika swali la msingi, Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir alitaka kujua tathmini ya mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu serikalini.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun  Ali  Suleiman amekiri kuwapo kwa changamoto kwa baadhi ya mifumo akieleza sababu kuwa ni pamoja na jambo hilo kuwa jipya.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho na wanaokumbana na changamoto hiyo wawalishe taarifa zao utumishi, na wapo ambao wanafanya hivyo na tatizo hilo linashughulikiwa.

“Jambo lolote likiwa jipya lazima liiibue changamoto, kwa hiyo hata mifumo hii bado ni mipya lakini Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha inamalizia jambo hili na imani yetu baada ya muda mfupi itakaa sawa,” amesema.

Kuhusu baadhi ya watumishi kupata kiwango kidogo cha mishahara, amesema wamelishughulikia na wapo waliowasilisha malalamiko yao na yameshafanyiwa kazi.

“Kuna hata wengine wameongezewa mishahara tunaomba nao waje waseme kwamba kiwango nilichopokea sio halali yangu, itakuwa jambo la busara,” amesema.

Kuhusu watumishi hewa, waziri huyo amesema bado Serikali inaendelea kufanya tathmini , ikikamilika  itatoa taarifa ya watu waliogundulika kulipwa mishahara hewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *