
Mfaransa Olivier Grondeau, ambaye amekuwa kizuizini nchini Iran tangu mwezi Oktoba 2022, “yuko huru, na ameunganishwa na familia yake nchini Ufaransa,” Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza siku ya Alhamisi, akihakikisha kwamba “uhamasishaji hautadhoofika” kwa ajili ya kuachiliwa kwa raia wawili wa mwisho wa Ufaransa ambao bado wako gerezani huko Tehran.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Tunashiriki furaha na familia yake,” rais wa Ufaransa amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X, akimzungumzia Olivier Grondeau, 34, ambaye alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela nchini Iran kwa kosa la ujasusi, hukumu ambayo ilionekana kuwa ya kiholela na viongozi wa Ufaransa, ambao wameshutumu Iran kwa kushikilia mateka raia wa nchi za kigeni.
“Ninashukuru idara zote za serikali, balozi wetu nchini Iran, na Kituo cha Mgogoro na Msaada cha Quai d’Orsay kwa hatua yao madhubuti,” ameongeza.
Rais hakutaja ni lini haswa raia huyo wa Ufaransa aliachiliwa huru au mazingira ya kuachiliwa kwake. Lakini kuachiliwa kwa raia huyo kumekuja baada ya mazungumzo marefu na magumu kati ya nchi hizo mbili na katika muktadha wa mzozo kati ya nchi za Magharibi na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia. Tehran inakanusha kuwa inataka kupata silaha za nyuklia, ingawa akiba yake ya uranium iliyorutubishwa inakaribia kizingiti kinachohitajika kuzizalisha.
Olivier Grondeau, ambaye anatimiza umri wa miaka 35 wiki ijayo, alipaswa kufanyiwa vipimo vingi kwani alikuwa amedhoofika sana katika miezi ya hivi karibuni, hasa kisaikolojia, chanzo cha serikali kimeliambia shirika la habari la AFP.
“Kuachiliwa kwa Olivier Grondeau ni heshima kwa diplomasia ya Ufaransa na kazi ngumu ya ubalozi wetu huko Tehran, kituo cha mgogoro na msaada, na idara za Wizara ya Mambo ya nje, ambao ninawapongeza kwa uvumilivu wao,” amesema mkuu wa diplomasia Jean-Noël Barrot, kwenye mtandao wa kijamii wa X “Tutaendelea bila kuchoka juhudi zetu za kuhakikisha kuwa raia wetu wote ambao wanashikiliwa mateka, ikiwa ni pamoja na Cécile Kohler naJacques Paris, wanaachiliwa.