
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Bushra Ali amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka 13, yakiwemo kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 4.6 (zaidi ya Sh10 bilioni).
Ali, amefikishwa katika mahakamani hapo leo, Aprili 30, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mhini alimueleza mshtakiwa kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia, shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Baada ya hakimu kutoa maelezo hayo, ndipo mshtakiwa aliposomewa mashtaka yake.
Kati ya mashtaka hayo 13; matano ni ya kughushi nyaraka, matano ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam, moja la kuongoza genge la uhalifu, jingine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kutakatisha fedha.
Akisomewa mashitaka yake na Wakili wa Mafuru, ilidaiwa kati ya Juni Mosi, hadi Novemba 30, 2024, jijini Dar es Salaam, akiwa na watu wengine, waliongoza genge la uharifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Wakili Mafuru alidai, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matano ya kughushi ambapo anadaiwa kugushi nyaraka iliyojulikana kama Delivery Order (original), kwa lengo kuonesha halisi imetolewa na Kampuni ya Nyota Tanzania Limited kwenda kwa wakala wao Maersk Group, akijua si kweli.
Iliendelea kudaiwa kuwa, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matano ya kuwasilisha nyaraka hiyo ya kugushi Bandari ya Dar es Salaam, akijifanya ni halali imetolewa na Kampuni ya Nyota Tanzania Limited kwenda kwa wakala wao Maersk Group, akijua siyo kweli.
Ilidaiwa kuwa, kati ya Juni Mosi, hadi Novemba 30, 2024, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo akiwa na watu wengine, alijipatia kilogramu 6,367,262 za mafuta ya kupikia aina ya camar ya thamani ya dola 4,627,459.14, mali ya Aastar Trading PTE LTD.
Ilidaiwa kuwa, alijipatia mafuta hayo baada ya kudanganya kuwa bili halisi ya wakala wa shehena ya mafuta hayo, imetolewa na Kampuni ya Nyota Tanzania Limited kwenda kwa wakala wake Mearsk Group.
Mshitakiwa huyo pia anakabiliwa na shitaka moja la utakatishaji fedha ambapo ilidaiwa kuwa, kwa vitendo hivyo, akishirikiana na watu wengine, alijihusisha na muamala wa dola 4,627,459.14, zilizoingizwa katika akaunti ya Matange Logistics and Trades company Limited, wakati akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kugusi.
Baada ya kusomwa mashitaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 5, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Mshitakiwa amepelekwa mahabusu kwasababu shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.