
Mwanza. Polisi mkoani Mwanza limemuachia kwa dhamana Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ huku uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ukiendelea.
Zumaridi, ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kugeuza makazi yake kuwa kanisa, kuendesha shughuli za kidini bila usajili, kuhubiri kwa sauti ya juu na kudaiwa kuaminisha watoto kuwa yeye ni mungu wao.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumamosi Mei 17, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema Zumaridi alikidhi masharti ya kisheria ya dhamana, na hivyo ameachiwa ikiwa ni haki yake ya kisheria.
“Mtuhumiwa alipewa dhamana siku hiyo hiyo (Mei 15, 2025), tulipomkamata, ambayo ni haki yake kisheria. Uchunguzi bado unaendelea,” amesema Mutafungwa.
Tuhuma za Zumaridi
Zumaridi, ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa jijini Mwanza, alikamatwa Mei 15, 2025 kutokana na tuhuma za kuendesha shughuli za kidini kwa sauti ya juu, huku akidaiwa kusababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, Zumaridi anadaiwa kuhubiri kwa watoto, akieleza kuwa yeye ni mungu wao na ana uwezo wa kuwaokoa na kifo, jambo ambalo lilijitokeza kupitia picha mjongeo zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Hii ni mara ya tatu kwa Zumaridi kuingia katika mgogoro na Serikali na Jeshi la Polisi. Novemba 18, 2019, kanisa lake lilifungwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi, kwa madai ya kuendesha ibada ambazo zilikiuka sheria ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutumia katiba ya kanisa lingine.
Februari 2022, alikamatwa kwa tuhuma za usafirishaji haramu wa binadamu, ambapo alikamatwa na watu 149, wakiwemo watoto 24 wenye umri kati ya miaka minne hadi 17.
Machi, 2022 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza yeye na wafuasi wake ambapo alisomewa mashitaka matatu ya kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao, kufanya mkusanyiko usio na kibali na usafirishaji haramu wa binadamu lililokuwa likimkabili Mfalme Zumaridi peke yake.
Hata hivyo, Desemba, 2022 Mahakama hiyo iliwaachia huru