Mfalme Charles III ameungama kuhusu “sura chungu” ya utawala wa kikoloni wa Uingereza duniani huku kukitolewa miito ya kulipwa fidia ya utumwa ulioendeshwa na mkoloni huyo mkongwe.
Mfalme wa Uingereza ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwa viongozi na wawakilishi wa mataifa 56 wanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) waliohudhuria mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa hayo (CHOGM) uliofanyika Samoa, nchi ya kisiwa iliyoko katika Bahari ya Pasifiki.
Akiashiria bila kuweka wazi utumwa wa zamani ulioendeshwa Asia, Afrika na Karibea wakati wa utawala wa kikoloni wa Uingereza, Charles alisema: “mshikamano wetu unahitaji kuungama na kutambua tulikotoka.”

Mfalme wa Uingereza alifafanua kwa kusema: “ninaelewa kutokana na kuwasikiliza watu katika jumuiya ya madola ni vipi sura zenye machungu makubwa zaidi za siku zetu zilizopita zinavyoendelea kutoa mtikisiko”; na akaongezea kwa kusema:
“kwa hivyo, ni muhimu kwamba tuelewe historia yetu, ili ituongoze kufanya machaguo sahihi katika siku za usoni ambapo kuna hali ya kukosekana kwa usawa”.
Charles amesisitiza kwa kusema: “hakuna yeyote kati yetu awezaye kubadilisha yaliyopita, lakini tunaweza kujikubalisha kwa mioyo yetu yote kuyafuata tunayojifunza ndani yake.”
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer pamoja na mwenzake wa Australia Anthony Albanese walikuwa miongoni mwa washiriki mwa mkutano huo wa CHOGM .
Licha ya kutoa msukumo wa kufanyika alichokiita “mazungumzo halisi” kuhusu kutolewa fidia ya utumwa na Uingereza, Starmer amekataa kuomba msamaha rasmi na pia utoaji wa fidia ya fedha kwa madhara ya utumwa uliotokana na ukoloni wa nchi yake…/