Kirsty Coventry, amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kuongoza kamati ya kimataifa ya Olimpiki, ambapo ametengeneza historia baada ya kuchaguliwa na nchi wanachama kuongoza taasisi hiyo, akiwashinda wagombea wengine 7.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kirsty Leigh Coventry Seward, amekuwa waziri wa Michezo wa Zimbabwe tangu mwaka 2018, alishinda medali mbili za olimpiki katika olimpiki tano alizoshiriki.
Kirsty, anamrithi Thomas Bach baada ya kuwapiku wagombea wengine sita kwa kujipatia kura 49 kati ya 97 katika raundi ya kwanza.
Mshindani wake wa karibu Juan Antonio Samaranch Jr alipata kura 28 huku mfaransa David Lappartient na Mjapani Morinari Watanabe wakipata kura nne kila mmoja na Prince Feisal al Hussein wa Jordan na Eliasch wa Sweden walipata kura mbili mbili.
Akizungumza baada ya ushindi wake, Kirstyamesema kuchaguliwa kwake ni ishara kuwa kamati ya olimpiki imekumbatia utafauti wa watu, michango na ataendelea kukuza hilo katika muhula wake wa miaka minane.
Coventry ambaye alikuwa mwogeleaji, tayari amekuwa kwenye bodi ya Olimpiki na kibarua chake cha kwanza kitakuwa ni mashindano ya olimpiki ya Milan Cortina mwezi Februari mwaka 2026.