Mfahamu King Kazu babu anayecheza Ligi ya Japan

Yokohama, Japan. NI mazoea kwa wanasoka wengi duniani wamekuwa wakiachana na soka mara baada ya kufikisha miaka 33, lakini mambo ni tofauti kwa Kazuyoshi Miura ambaye ameishangaza dunia.

Mshambuliaji huyo wa klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Japan, Atletico Suzuka ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza soka kwa sasa akiwa na  miaka 57 akitarajiwa kufikisha 58, Februari mwakani.

Pamoja na kufikisha umri huo, bado nyota huyo ambaye anajulikana kwa jina maarufu la King Kazu ameshasema kuwa hana mpango wa kustaafu soka kwa sasa.

Staa huyo msimu huu ameshacheza mechi 10 za Ligi Kuu ya Japan, huku akitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji ambao wanaonyesha kiwango cha juu uwanjani, ana kasi, chenga za maudhi na uwezo wa juu wa kupiga mashuti.

 Kazuyoshi anatarajiwa kuutumikia msimu wa 40 kwenye soka kwa sasa akiwa anawashangaza wengi kutokana na jinsi ambavyo amekuwa akipambana na wachezaji wenye umri mdogo uwanjani.

Taarifa zinaonyesha kuwa wale ambao aliwahi kucheza nao akiwa na umri wa miaka 19 wameshaachana na soka miaka 10 na zaidi iliyopita, hata hivyo, ni wachezaji wachache tu wenye miaka zaidi ya 40 ambao bado wanacheza kwa sasa.

Baadhi yao ambao wanacheza baada ya kufikisha miaka 40 lakini hawajafikia rekodi ya Kazuyoshi ni pamoja na Staa wa Peru Paolo Guerrero (ambaye anafikisha miaka 41 Januari mwakani), nyota wa Paraguay Roque Santa Cruz (43), pamoja na Mbrazil Felipe Melo (41), huku mshindi wa Ballon d’Or Cristiano Ronaldo (akitarajiwa kufikisha miaka 40 Februari mwakani).

Kwa Tanzania ni wachezaji wachache ambao waliwahi kucheza wakiwa na umri wa miaka 40 na zaidi mmoja wao akiwa mshambuliaji, Madaraka Suleimani ambaye aliitumikia Simba akiwa na miaka 41.

Miura ambaye bado anaonekana kuwa na umbo safi la kiuanamichezo, amekuwa akisema mara kwa mara kuwa anataka kucheza soka la ushindani hadi atakapofikisha miaka 60 na anajiandaa kupambana kwa nguvu zote ili kufikia malengo hayo.

Akiwa na jina la utani la’King Kazu’ alianza kucheza soka la ushindani mwaka 1986 akitumikia Santos ya Brazil ikiwa ni klabu hiyo hiyo ambayo ilimuibua staa mkubwa duniani Pele. Aliitumika hapo kwa misimu minne na kurudi Japan ambapo alitwaa MVP mwaka 1993 akiwa anaitumikia Verdy Kawasaki.

Msimu wa 1993-1994, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Bara la Asia kucheza Ligi Kuu ya Italia, Seria A, ambapo alijiunga na Genoa CFC kwa kipindi alichokaa hapo alifunga bao moja tu kwenye michezo 21, lakini alikuwa akitumika kama kiungo na sio mshambuliaji sehemu ambayo ameizoea kucheza kwa muda mrefu.

Hata hivyo, kwenye mahojiano yake mengi ambayo amekuwa akifanya mara kwa mara amesema hatasahau mchezo wa ligi hiyo walipovaana na AC Milan ambapo alipata majeraha ya kichwa na kuvunjika pua baada ya kugongana na Franco Baresi na jeraha hilo lilimweka nje kwa muda mrefu na wengi waliamini kuwa ndio mwisho wa maisha yake ya soka.

“Nafikiri ajali ya uwanjani dhidi ya Franco Baresi ndiyo jambo ambalo nalikumbuka la kushtua zaidi kwenye soka hadi sasa, watu wengi waliamini kuwa ndio maisha yangu ya soka yamefika mwisho lakini wengine wanashangaa kuniona hadi leo hii nacheza,” alisema mkongwe huyo.

Baadae staa huyo alijiunga na timu kutoka Croatia ya Dinamo Zagreb ambayo aliitumikia kwenye michezo 12 bila kufunga bao lolote na kurudi kwao kujiunga na Yokohama FC.

Hata hivyo, timu hiyo ndiyo ilimpa umaarufu mkubwa ambapo amecheza kwa misimu 16 hadi sasa, akicheza michezo 293 na kufunga mabao 27.

Anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye heshima kubwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Japan akiwa ametumika hapo kwa miaka 11 akicheza michezo 89 na kufunga mabao 55.

Nyota huyo aliyezaliwa mwaka 1967, alifahamika zaidi mwaka 1992 alipoiwezesha nchi yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Asia ‘Asian Cup’ akiwa na jezi namba 11 ambapo alitajwa kama mchezaji bora wa michuano hiyo.

Hata hivyo, kwenye mafanikio ya makombe timu ya Tokyo Verdy ndiyo aliyotwaa nayo makombe mengi baada ya kuchukua tisa.