Katika taarifa, chama cha CHP kilisema Imamoglu na timu yake ya mawakili hawatohudhuria kikao cha mahakama cha Alhamis kutokana na kubadilishwa kwa eneo litakakofanyika kesi hiyo, kwa njia zisizo za kisheria.
Akizungumzia kupitia chapisho aliloweka mtandaoni kutoka jela, Imamogluamesema “kikao hicho cha mahakama si cha kawaida na hakiendani na misingi ya kesi hiyo na kwamba anakataa kuwa sehemu yake.”
Kesi ya Alhamis ambayo ilikuwa inahusu matamshi aliyoyatoa Imamoglu kuhusiana na kufunguliwa mashtaka kwa maafisa wengine kutoka chama chake cha Republican People’s Party, CHP, ni mojawapo ya mashtaka ya jinai yanayomkabili Imamoglu.
Meya huyo alikamatwa mnamo mwezi machi pamoja na wanasiasawengine wakuu kama sehemu ya uchunguzi kuhusiana na madai ya ufisadi na kuhusishwa na ugaidi.
Maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa Uturuki
Kukamatwa kwake kulisababisha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa katika mitaa ya nchini Uturuki katika kipindi cha mwongo mmoja.
Iwapo Imamoglu atapatikana na hatia na kuhukumiwa katika mojawapo ya kesi hizo basi huenda akapigwa marufuku ya kushikilia au kugombea wadhfa wa umma.
Imamoglu anachukuliwa kama mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan aliyeitawala Uturuki kwa miaka 22 na alichaguliwa rasmi kama mgombea urais wa chama chake kufuatia kufungwa kwake.
Kulingana na tafiti za maoni, watu wengi nchini Uturuki wanachukulia kesi zinazomkabili Imamoglu kama za kubambikiwa tu na kwamba siasa zina mkono katika kesi hizo.
Uchaguzi ujao Uturuki utakuwa mwaka 2028 ila huenda ukafanyika karibuni.