KIPA wa Singida Black Stars, Metacha Mnata amesema ufundi wanaouonyesha makipa Moussa Camara (Simba) na Djigui Diarra(Yanga) ni funzo kwa wazawa kuboresha viwango vyao, ili thamani zao kupanda.
Metacha aliyewahi kuichezea Yanga kwa nyakati tofauti, Azam FC, Ihefu na Taifa Stars, alisema Camara na Diarra wana uwezo wa kuamua matokeo, kutuliza presha ya timu, viongozi dhidi ya wachezaji wenzao na wanajua kuwapanga na kuelewana na mabeki.
“Alianza Diarra kuonyesha utofauti akiwa golini mfano kuanzisha mashambulizi, umakini wa kuokoa hatari katika hali ya utulivu na kuifanya timu isicheze kwa presha, jambo ambalo lilikuwa linampa umarufu na kupendwa na mashabiki wake na kitu nilichokuwa nakipenda zaidi kutoka kwake akidaka mpira alikuwa anawasoma kwanza wachezaji wenzake ndipo anaanzisha mashambulzi,” alisema Metacha ambaye ana clean sheets sita na kuongeza;

“Ujio wa Camara umeendelea kuonyesha eneo la kipa kuwa la burudani kwani anajiamini na siyo mrahisi kumfunga, kulingana na jinsi ambavyo anapanga mabeki wake, anaweza kuokoa mipira ya kushitukiza, lakini hilo halimanishi kama makipa wazawa hawana jambo la kujivunia kutoka kwao, mfano kipindi kina Juma Kaseja, Ivo Mapunda ukiacha wale ambao hatujawashuhudia tunasikia sifa zao, walikuwa wanacheza kwa kiwango cha juu sana.”
Alisisitiza siyo dhambi kwa makipa wazawa kujifunza mbinu na ufundi walionao Camara na Diarra kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani na kupandisha thamani zao, zitakazowafanya wawe ghari sokoni.
Ukiachana na alichozungumza Metacha aliyekuwa beki wa Yanga, Juma Abdula naye kamzungumzia Camara kuongeza thamani ya eneo la kipa kuingia katika ushindani kama zilivyo nafasi za ndani.
“Binafsi ukiacha kuvutiwa na wanachokifanya wachezaji wa ndani, akiwepo Camara golini napenda kumuangalia na jinsi anavyowapa wakati mgumu washambuliaji kulifikia goli lake, hicho ni kitu kizuri hata akifungwa mfungaji anasifiwa,” alisema.

TAKWIMU ZAO
Camara amedaka mechi 20 akiwa na clean sheet 15, karuhusu mabao katika michezo tano dhidi ya Coastal Union (mabao 2-2,Oktoba 4, 2024), dhidi ya Yanga (bao moja Oktoba 19,2024), Fountain Gate (bao 1-1, Februari 6, 2025), dhidi ya Azam (mabao 2-2 Februari 24,2024) na dhidi ya Kagera Sugar na Simba ilishinda kwa mabao 5-2, mchezo huo ulipigwa Desemba 21,2024, hivyo kacheza jumla ya dakika 1,800, kafungwa mabao manane.
Kwa upande wa Diarra kacheza mechi 16 akipata clean sheet 11, kafungwa mabao sita akicheza dakika 1,440.