Messi avamiwa uwanjani, bodigadi akizidiwa ujanja

Miezi 11 baada ya kupata sifa ya kumlinda Lionel Messi dhidi ya kuvamiwa na shabiki uwanjani, jana Jumapili, Februari 02, 2025 mambo yalienda tofauti kwa mlinzi maalumu wa nahodha huyo wa Argentina, Yassine Chueko.

Hiyo ni kufuatia kitendo cha shabiki mmoja kumzidi ujanja na kumvamia Messi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Sporting San Miguelito.

Shabiki huyo alitumia ujanja wa kuingia uwanjani kwa kuruka kwenye eneo la kuchezea akipitia upande wa goli mojawapo na kukimbilia mahali alipokuwa Messi.

Picha zilizosambaa katika mitandao ya kijamii, zimemuonyesha Chueko akikimbia kwa kasi kumuwahi shabiki huyo ili asimfikie Messi.

Pamoja na kufanikiwa kumuwahi, Chueko alianguka baada ya kushikwa usoni na shabiki huyo ambaye naye aliteleza.

Hata hivyo Chueko alifanikiwa kumdhibiti shabiki huyo na kumtoa kwa  Messi ambapo ameonekana kama mtu aliyepigwa na butwaa.

Chueko amejizolea sifa nyingi, baada ya Aprili mwaka jana kufanikiwa kumuwahi shabiki ambaye aliingia uwanjani kwa lengo la kutaka kumkumbatia nyota na nahodha huyo wa Inter Miami.

Chueko ni mlinzi maalumu wa Messi ambaye alipewa na mmiliki wa timu hiyo, David Beckham muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo.

Mlinzi huyo amewahi kuwa Askari wa Jeshi la Anga la Marekani ambaye ameshiriki katika vita ya Iraq na Afghanistan.

Amekuwa akishiriki pia katika sanaa za mapigano, ngumi pamoja na mapambano ya MMA.