Merz aonya ushuru wa Trump kuuathiri uchumi wa Ujerumani

Merz aonya ushuru wa Trump kuuathiri uchumi wa Ujerumani

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Rais Donald Trump, Merz alisema walijadili kwa kina masuala ya biashara na ushuru pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano.

Aidha, alielezea kuwa mkutano huo ulikuwa na mafanikio, na pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika masuala hayo muhimu.

Merz alibainisha kuwa walijadili pia mchango wa viwanda vya magari vya Ujerumani vilivyoko Marekani, na kusema atatuma maafisa wake kuendeleza majadiliano hayo kwa undani zaidi, akiongeza kuwa Ujerumani, kama nchi inayoongoza kwa mauzo ya nje, ina wajibu mkubwa katika sera za biashara za Umoja wa Ulaya.

“Tumekubaliana kwamba kutakuwa na ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na sera ya biashara kati ya White House na ofisi ya kansela. Tayari tumeteua watu watakaoshughulikia mazungumzo haya kwa niaba yetu, na kuyapa kasi zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Tunaliendeleza tena jambo hili na kuyaimarisha mazungumzo hayo,” alisema Merz.

USA Friedrich Merz
Kansela Merz aliwaambia waandishi habari kwamba anaamini mazungumzo kati yake na Rais Trump yalikuwa ya manufaa makubwa.Picha: DW

Rais Trump ameupa Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa kibiashara muda hadi Julai 9 kufikia makubaliano, la sivyo Marekani itaanza kutoza ushuru mkubwa zaidi.

Tayari EU inakumbwa na ushuru wa asilimia 50 kwenye bidhaa za chuma na alumini na asilimia 25 kwenye magari. Ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa, bidhaa nyingine zinaweza kutozwa ushuru wa hadi asilimia 50.

Merz aliviambia vituo vya CNN na Fox News kwamba ushuru huo una athari kubwa kwa watengenezaji wa magari wa Ujerumani, na kusisitiza kuwa sera za biashara huria na masoko wazi ndio njia bora ya kuhakikisha ustawi wa pamoja wa nchi hizo mbili.

Alitoa mfano wa magari 400,000 yanayotengenezwa na makampuni ya Ujerumani nchini Marekani, idadi inayolingana na uzalishaji wa ndani ya Ujerumani, na baadhi ya magari hayo hurudishwa tena Ujerumani kama bidhaa za kuuza nje.

Akosolewa kuwabebsha Waislamu na wahamiaji lawama

Kwa upande mwingine, Merz pia alizungumzia changamoto ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.

Katika mahojiano na kituo cha Fox News, alisema kwamba uhamiaji mkubwa ulioshuhudiwa katika muongo mmoja uliopita umechangia kuibuka kwa kile alichokiita “chuki iliyoingizwa kutoka nje.”

Kauli hiyo imezua mjadala mkali nchini Ujerumani, ambapo wakosoaji wanasema inawalenga Waislamu na wahamiaji huku ikipuuza mizizi ya chuki hiyo ndani ya jamii pana ya Ujerumani.

Riwaya za uwongo kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Takwimu zilizotolewa na shirika la RIAS wiki hii zinaonyesha ongezeko la asilimia 77 la visa vya chuki dhidi ya Wayahudi mwaka 2024, ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kati ya visa 8,627 vilivyoripotiwa, zaidi ya 5,800 vilihusiana na mzozo wa Israel, ambapo Wayahudi waishio Ujerumani walibebeshwa lawama kwa matendo ya serikali ya Israel.

Merz alisema serikali yake inachukua hatua kali dhidi ya wale wanaovunja sheria na kuhusika katika matendo hayo ya chuki.

Alisisitiza kuwa juhudi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa idadi ya matukio kama hayo inapungua, na kwamba Ujerumani itaendelea kusimama kidete kulinda haki na usalama wa Wayahudi nchini humo.

Sources: DPA, RTRE, AFPE

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *