Medvedev aonya: Kombora la Oreshnik linaweza kusababisha uharibifu Magharibi kwa dakika chache

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia, amesema kwamba kombora la nchi hiyo la “Oreshnik” linaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa miji mikuu ya Magharibi ndani ya dakika chache, akitoa wito kwa Ulaya kuacha kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Dmitry Medvedev ameongeza kuwa, “Ulaya inajiuliza ni uharibifu gani mfumo wa Oreshnik unaweza kusababisha ikiwa utakuwa na vichwa vya nyuklia, iwapo inawezekana kutungua makombora haya na kuhusu kasi yake ya kufika katika miji mikuu ya dunia kongwe.”

Amesisitiza kuwa “uharibifu utakuwa mkubwa, na haiwezekani kutungua kombora hilo kwa kutumia njia za kisasa. Tunazungumza juu ya dakika,” akibainisha kuwa “maficho hayatasaidia lolote, na tumaini pekee ni kwa Russia kutoa onyo la mapema kabla yakurushwa kombora “Oreshnik.”

Haya yanajiri baada ya taarifa zilizotolewa na msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, Dmitry Peskov akithibitisha kwamba makabiliano ya sasa yanachochewa na nchi za Magharibi, akionyesha kwamba amri ya kusasisha Mwongozo wa Myuklia ya Rais Vladimir Putin inaweza kutambuliwa kuwa ishara kwa Magharibi.

Jumanne iliyopita, Rais Vladimir Putin wa Russia alitia saini amri ya kupanua uwezekano wa nchi yake kutumia silaha za nyuklia, na kusema kuwa Moscow huenda ikafikiria kutumia silaha hizo iwapo itakabiliwa na shambulio la kombora la kawaida linaloungwa mkono na nchi inayomiliki silaha za nyuklia.