
Siku chache baada ya kuachana na Kagera Sugar, kocha Melis Medo ameibukia Singida Blacks Stars akiajiriwa katika nafasi ya kocha msaidizi.
Medo ameachana na Kagera Sugar mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi katika siku za hivi karibuni.
Taarifa iliyotolewa na Singida Black Stars leo, Jumanne, Februari 25, 2025 imeeleza kuwa Medo atakuwa miongoni mwa makocha watatu wasaidizi ndani ya timu hiyo.
“Uongozi wa klabu ya Singida Black Stars unaendelea kufanya maboresho katika benchi la ufundi na sasa umefikia makubaliano na kocha Melis Medo ambaye atakuwa kocha msaidizi na mshauri wa benchi la ufundi, sambamba na Kocha Juan Magro wakisaidiwa na Kocha Muhibu Kanu.
“Timu itaendelea kuwa chini ya kocha mkuu, David Ouma.
“Maboresho haya yanalenga kujiimarisha zaidi kufikia malengo ya klabu ikiwemo kuhakikisha tunapata tiketi ya kufuzu na kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao,” imefafanua taarifa ya Singida Black Stars.
Medo alifikia makubaliano ya kuachana na Kagera Sugar baada ya timu hiyo kupoteza mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Februari 21 kwa mabao 2-0.
Kabla ya hapo, Kagera Sugar ilikuwa imepata ushindi katika mechi moja tu kati ya 10 ilizocheza, ikipata sare nne na kupoteza tano.