Mechi za ugenini mwiba Ligi Kuu Bara

Kupata ushindi ugenini limekuwa sio jambo rahisi katika soka la Afrika na hilo linaweza kujidhihirisha katika Ligi Kuu ya NBC msimu unaoendelea wa 2024/2025.

Pamoja na maandalizi mazuri ambayo timu zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu zimeyafanya kabla ya kuanza kwake, viwanja vya ugenini vimeonekana kuwa vigumu kuvuna ushindi kulinganisha na vile vya nyumbani.

Timu nyingi zimekusanya idadi kubwa ya pointi nyumbani kuliko ugenini lakini hata kufunga mabao, zimekuwa zikifanya hivyo kwa ufasaha pindi zinapokuwa nyumbani na pia hilo linaweza kujidhihirisha hata kwa uimara wa kiulinzi pindi zinapokuwa nyumbani kulinganisha na ugenini.

Lakini sio timu tu bali hata wachezaji wamekuwa na takwimu nzuri katika upande wa ufungaji na ulinzi pindi wanapocheza katika viwanja vya nyumbani na wanapokuwa ugenini wamekuwa wakikutana na ugumu.

Wanyonge wengi

Ni timu chache tu ambazo zimefanikiwa kupata ushindi katika idadi kubwa ya mechi za ugenini msimu huu huku nyingi zikipoteza ama kwa kuangusha pointi zote tatu au kudondosha pointi mbili.

Kabla ya mechi za jana juzi, ni timu tano tu ambazo kila moja ilikuwa imepata ushindi zaidi ya mara mbili ugenini huku nyingine 11 zikishindwa kufanya hivyo licha ya kila moja kucheza zaidi ya mechi nne ugenini.

Yanga, Singida Black Stars, Simba, Azam na Fountain Gate ndio timu pekee ambazo angalau kila moja ilikuwa imepata ushindi ugenini zaidi ya mara mbili, Mashujaa, Namungo, Tabora United na KMC zikiwa ndio ambazo angalau zimepata ushindi mara moja katika viwanja vya ugenini na zilizobakia zimeshindwa kufanya hivyo.

Timu tatu hadi sasa zina ushindi wa asilimia 100 kwa mechi za ugenini kila moja ambazo ni Yanga iliyopata ushindi katika mechi zote tano ilizocheza ugenini na kuna Simba na Singida Black Stars ambazo kila moja imepata ushindi katika mechi zote nne ambazo kila moja imecheza ugenini.

Azam FC hadi sasa imecheza michezo sita ugenini ambapo kati ya hiyo, mechi nne imepata ushindi na mechi mbili imepata matokeo ya sare.

Dodoma Jiji, JKT Tanzania, Tanzania Prisons, Kagera Sugar, Pamba Jiji na KenGold ni timu ambazo hadi sasa, ushindi wa mechi za ugenini za ligi kuu zinausikia hewani na hazijawahi kuuonja.

Mabao yakauka

Hadi sasa hakuna timu yoyote ambayo ina wastani wa kufunga angalau mabao mawili kwa mchezo pindi inapokuwa ugenini.

Mashujaa ndio timu yenye wastani mzuri wa mabao ya ugenini ambapo inapata wastani wa bao 1.7 kwa mchezo ikifuatiwa na Singida Black Stars yenye wastani wa bao 1.5 huku Fountain Gate ikishika nafasi ya tatu ikiwa inafunga wastani wa bao 1.4 katika mechi ya ugenini.

Simba ipo nafasi ya nne ikiwa inafunga wastani wa bao 1.3 ugenini sawa na Azam FC na Yanga iko nafasi inayofuata ikiwa inafunga wastani wa bao 1.2 ugenini.

Timu ambazo safu zao za ushambuliaji ni butu zaidi ugenini ni Pamba Jiji na Tanzania Prisons ambazo hadi sasa hazijafunga bao lolote katika ligi hivyo.

Ukiondoa hizo, timu nyingine zenye wastani kiduchu wa kufumania nyavu ugenini ni JKT Tanzania ambayo inafunga wastani wa bao 0.2 ugenini na Namungo FC ambayo hadi sasa katika mechi za ugenini ina wastani wa kufunga bao 0.4 kwa mchezo.

Dodoma kinara sare

Matokeo ya sare ugenini yanaonekana kuiandama zaidi Dodoma Jiji kuliko timu nyingine yoyote kwenye Ligi Kuu hadi sasa.

Dodoma Jiji imetoka sare mara tano katika mechi sita ilizocheza ugenini ikifuatiwa na Tanzania Prisons ambayo katika mechi nne za ugenini, imetoka sare tatu na kupoteza moja.

Timu sita hazijawahi kuonja ladha ya matokeo ya sare ugenini msimu huu ambazo ni Yanga, Singida Black Stars, Simba, Fountain Gate, Namungo na KenGold.

Wachezaji wakiona

Hadi sasa mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao ugenini ni nyota wa Fountain Gate, Edgar William ambaye amefumania nyavu mara tatu huku akifuatiwa na wachezaji nane tu waliofunga mabao mawili kila mmoja.

Wachezaji nane ambao wamefunga mabao mawili ugenini kila mmoja ni Seleman Mwalimu wa Fountain Gate, Emmanuel Kayekeh (Singida Black Stars), Iddi Selemani, Nassor Saadun na Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Daruwesh Saliboko (KMC), Richard Ulomi (Mashujaa) na Joshua Ibrahim (KenGold).

Sababu hizi hapa

Kocha wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah ‘Baresi’ alisema kuwa kukua kwa ligi ndio kunafanya timu zipate matokeo yasiyoridisha ugenini.

“Ligi yetu imepiga hatua kubwa hivi sasa na timu zinajiandaa vilivyo hasa zinapokuwa nyumbani kwa vile zinakuwa zinapata faida ya kucheza na mashabiki wao lakini hata hivyo ushindani upo kotekote kwa maana ya nyumbani na ugenini.

“Ukiangalia kwa sasa timu inaweza kupoteza hata nyumbani na ikashinda ugenini kwani kinachoamua ni ubora tu na aina ya maandalizi ambayo timu imeyafanya,” alisema Baresi.

Kocha wa Pamba, Felix Minziro alisema kuwa inawezekana timu ikapata matokeo mazuri ugenini ikiwa itafanya maandalizi mazuri.

“Lolote linawezekana na hakuna timu ambayo ina uhakika wa kupata ushindi nyumbani au ugenini kutokana na ubora wa timu ambazo zinashiriki ligi msimu huu. Binafsi nafurahishwa na ushindani uliopo kwenye ligi yetu kwa sasa kwani una faida kubwa kwa nchi yetu,” alisema Minziro.