Mechi za mwisho zinavyoibeba Stars kufuzu Afcon

Timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars, itashuka dimbani leo Novemba 19, 2024 dhidi ya Guinea kwenye mchezo wa mwisho wa makundi wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazo fanyika mwaka 2025 Morocco.

Stars ipo kundi H pamoja na DR Congo inayoongoza kundi kwa pointi 12, Guinea inashika nafasi ya pili kwa pointi tisa, wakati Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba huku Ethiopia ikiburuza mkia ikiwa na pointi moja.

Mara ya mwisho Tanzania kukutana na Guinea ilikuwa ni Septemba 10, 2024 ambapo Tanzania ilitoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ugenini.

Mara ya kwanza Stars ilifuzu kwenda Afcon ilikuwa mwaka 1980 ambapo ilifanikiwa kuiondosha Zambia kwenye hatua ya mtoano kwa jumla ya mabao 2-1 ambapo mechi ya kwanza ilichezwa Agosti 11, 1979, Stars ilishinda bao 1-0 ikiwa nyumbani na mchezo wa pili ulipigwa Zambia ambapo ilipata sare ya bao 1-1.

Machi 24, 2019 Stars ilifuzu kwenda Afcon kwa mara ya pili ilipoifunga Uganda mabao 3-0 kwenye mchezo wa mwisho ambapo ilimaliza nafasi ya pili kwenye kundi L ikiwa na pointi nane mbele ya Lesotho iliyomaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita wakati Cape Verde iliburuza mkia ikiwa na pointi tano huku Ugunda ikimaliza vinara ilipokusanya pointi 13.

Msimu uliyopita Stars ilienda Afcon kibabe baada ya kupata sare kwenye uwanja mgumu wa ugenini dhidi ya Algeria ambapo iliizidi Uganda pointi moja kwenye kundi F ikiibuka nafasi ya pili ikiwa na alama nane wakati Uganda ilikuwa na alama saba.

Hata hivyo, matokeo ya mechi za mwisho yanaonekana kuibeba Stars katika kuisaka tiketi ya kuwania kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) ambapo leo itakuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Guinea.

Stars inatafuta tiketi ya kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mara ya nne ambapo imefanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2022.