Mechi za moto Premier League wikiendi hii

Mchakamchaka wa Ligi Kuu England unarejea wikiendi hii kwa mechi za kibabe kabisa, ikiwamo ya huko Etihad, ambapo Manchester City itapomaliza ubishi na Chelsea.

Man City imetoka kukumbana na kipigo kizito kutoka kwa Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumfanya kocha wa miamba hiyo, Pep Guardiola kukiri kwamba timu yake kwa sasa haiwezi kucheza na timu kubwa. Je, Chelsea yenye mastaa wenye kasi kubwa uwanjani wataendeleza kipigo kwa Guardiola? Majibu ya swali hilo yatapatikana usiku wa leo Jumamosi huko Etihad.

Takwimu zinaonyesha kwamba Man City na Chelsea zimekutana mara 55 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, ambapo katika mechi hizo vigogo hao wametoka sare mara tisa.

 Hata hivyo, The Blues ndiyo watemi wa mechi hizo, ambapo mara 55 walizokutana kwenye ligi, Chelsea imeshinda 27, mara 14 ilipokuwa nyumbani Stamford Bridge na mara 13 ilipokwenda kuwakabili Man City uwanjani Etihad.

Man City yenyewe imeshinda mara 19 tu, ambapo 11 ilipocheza nyumbani na minane ilipokwenda ugenini kwa Chelsea. Namba hizo zinathibitisha kwamba, Chelsea imeshinda mara nyingi kwenye uwanja wa Man City, kuliko wenyeji hao, wakishinda kwa mechi mbili zaidi, huku kipute hicho kitawakutanisha watu wawili waliowahi kuwa pamoja Etihad, Enzo Maresca wa Chelsea na Guardiola wa Man City.

Ukiweka kando kipute hicho cha Etihad, Ligi Kuu England itashuhudia vita muhimu zaidi kwa msimu huu kwa timu zile zinazofukuzia ubingwa, ambapo Liverpool na Arsenal zote zitaingia uwanjani.

Liverpool itakuwa nyumbani Anfield kujaribu kutanua pengo la pointi na kufikia tisa kileleni ili kuwakatisha tamaa wapinzani wao wanaowafukuzia kwenye mbio za ubingwa wakati itakapomenyana na Ipswich Town, wakati Arsenal yenyewe itakuwa ugenini kuwakabili Wolves huko uwanjani Molineux.

Kwenye mbio za ubingwa, Liverpool na Arsenal zimetofautiana pointi sita tu kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo huku vijana wa Anfield wanaonolewa na Arne Slot wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya The Gunners ya Mhispaniola, Mikel Arteta.

Kwenye rekodi zinavyosoma ni kwamba Arsenal na Wolves zimekutana mara 21 katika mechi za Ligi Kuu England, ambapo mara tatu tu ndiyo mechi zilimalizika kwa sare, huko wenyeji wa mchezo huo wa leo, Wolves ikiwa imeshinda mara tatu, mbili ilipocheza nyumbani na moja tu ugenini. Arsenal ni wababe kwa Wolves unaweza kusema hivyo baada ya wenyewe kushinda mara 15, huku mechi saba walifanya hivyo wakiwa nyumbani na nane ugenini.

Kwa upande wa Liverpool mechi yao na Ipswich inaonekana kama ya upande mmoja, lakini kinachovutia ni kwamba katika mechi ambazo Ipswich iliwahi kushinda dhidi ya Liverpool ilifanya hivyo uwanjani Anfield, tena mara mbili.

Kwa ujumla wake, Liverpool na Ipswich zimekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, ambapo sare ni tatu huku Liverpool ikipata ushindi mara sita, mbili nyumbani na nne ugenini. Hapa kuna kazi.

Vipute vingine vya ligi hiyo yenye ushindani mkali utazishuhudia Bournemouth itakayokuwa ugenini kukabilisna na Nottingham Forest, ambayo imekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu.

Kipute hicho cha uwanjani Vitality  kitachagizwa na takwimu tamu kabisa za mechi za Bournemouth na Nottingham Forest, ambapo timu hizo mara tano ilizokutana kwenye Ligi Kuu England, Forest haijawahi kushinda mechi yoyote, huku tatu zikimalizika kwa sare. Na kinachovutia ni kwamba hata ushindi wa Bournemouth iliyopata dhidi ya Forest kwenye mechi zilizopita za Ligi Kuu England, haijawahi kushinda nyumbani kwa maana ya uwanjani Vitality. Mechi mbili ilizoshinda ilifanya hivyo nyumbani kwa Forest.  Je, safari hii itakuwaje? Bournemouth itashinda kwa mara ya kwanza Vitality Stadium au Forest itapata ushindi wake wa kwanza kwenye mechi za wawili hao? Kibabe sana.

Brighton ikitokea kuichapa Manchester United uwanjani Old Trafford itakuwa nyumbani kuikaribisha Everton ya kocha David Moyes katika moja ya mechi zinazotarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Everton imetoka kushinda mechi yao iliyopita walipoichapa Tottenham Hotspur 3-2, hivyo itaifanya Brighton ikiwa na mzuka kwelikweli wa kutafuta ushindi mwingine ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Mechi za Brighton na Everton kwenye Ligi Kuu England ni za piga nikupige, ambapo mara 15 walizokutana kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England, sare ni nne huku Brighton ikishinda tano na Everton imeshinda sita.

Katika mechi za Brighton, ilishinda mara mbili nyumbani na tatu ugenini, huku Everton yenyewe ikishinda nne nyumbani na mbili ugenini. Namba hizo ndicho kitu kinachofanya mechi ya Brighton na Everton kuwa na mvuto.

Kipute kingine cha Ligi Kuu England kitahusisha Southampton itakayokuwa nyumbani St Mary’s kukipiga na Newcastle United, ambayo ipo kwenye vita ya kusaka nafasi ndani ya Top Four ili kukamatia tiketi ya kucheza mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Moto wa Ligi Kuu England utaendelea kesho Jumapili, ambapo Crystal Palace itakuwa nyumbani Selhurst Park kucheza na Brentford, huku Spurs itajimwaga kwao huko London kukabiliana na Leicester City.

Macho ya wengi yatakuwa huko Spurs kuona kama kuna jambo jipya itafanya kwenye mchezo huo wa kuwakabili Leicester City, ambao kwa takwimu zao zinavyosoma kutokana na mechi walizowahi kukutana kwenye Ligi Kuu England, 35 mara sita zilimalizika kwa sare, huku Spurs ikishinda 16, tisa nyumbani na saba ugenini, wakati Leicester City yenye maskani yake King Power, imeshinda 13, mara nane nyumbani na tano ugenini.

Aston Villa ya Unai Emery itakuwa kwao Villa Park kukipiga na West Ham United katika moja ya mechi za upinzani mkali kwenye Ligi Kuu England, huku shughuli pevu nyingine itakuwa huko Craven Cottage, ambapo Fulham itakuwa na kibarua kizito cha kuikabili Man United.

Wengi watasubiri kuona kama Ruben Amorim atabadili hali ya mambo kwenye kikosi cha Man United baada ya kupoteza kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu England kabla ya kwenda kuichapa Rangers 2-1 kwenye Europa League usiku wa juzi Alhamisi. Takwimu zinaonyesha Man United imekuwa mtawala wa mechi dhidi ya Fulham, iwe inacheza ugenini au nyumbani kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Mara 35 ambazo timu hizo zilikutana, Fulham imeshinda nne tu, mbili nyumbani na mbili nyingine ugenini, huku sita zikimalizika kwa sare na Man United yenyewe imeshinda 25, mara 14 nyumbani na 11 ugenini. Man United inahitaji ushindi ili kujiondoa kwenye hatari ya kutumbukia kwenye shimo la kushuka daraja, huku ikijaribu kusaka pointi pia za kuwafanya kuingoa kwenye Top Four ili kuchuana kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.