Mechi tano za Chippa United bila Majogoro

WAKATI Chippa United ya Afrika Kusini anayeichezea Mtanzania, Baraka Majogoro ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi baada ya michezo 15, nyota huyo amekosekana katika michezo mitano ya mwisho.

Majogoro anabakia kuwa Mtanzania pekee kwenye ligi hiyo baada ya Abdi Banda aliyekuwa anakipiga Baroka FC kurudi Bongo na kutua Dodoma Jiji, huku Gadiel Michael akienda zake Singida Black Stars.

Januari mwaka huu zilizuka taarifa kutoka mitandao mbalimbali nchini Afrika Kusini, nyota huyo amevunja mkataba kwa makubaliano maalumu na Chippa lakini baadae akasema hana taarifa hizo anachojua yeye ni mchezaji halali.

Mechi tano za mwisho ilizocheza timu hiyo kiungo huyo fundi wa zamani wa KMC hakuwepo hata benchi na mara ya mwisho kucheza ni Desemba 26 dhidi ya Kaizer Chiefs iliyoshinda bao 1-0 huku nyota huyo akicheza kwa dakika 56.

Huu unakuwa msimu wa pili kwa Majogoro kuitumikia timu hiyo na msimu uliopita alionyesha kiwango bora kiasi cha kubeba na tuzo za mchezaji bora wa mwezi, akicheza mechi 16 za mashindano na msimu huu unaokaribia ukingoni amecheza nane.