Mechi saba Adebayor haoni maajabu

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Victorien Adebayor bado hajajipata huku akieleza haoni kama kuna maajabu yanaweza kutokea katika mechi saba zilizosalia kufunga msimu huu.

Adebayor ambaye hajafunga bao wala kutoa asisti katika Ligi Kuu Bara msimu huu, alisema hata akipata nafasi ya kucheka na nyavu kwa mechi zilizosalia hazimaanishi kuna maajabu makubwa anayoyatarajia kuyaona ama kuyafanya kwa ligi ilipofikia.

“Ukiniuliza matarajio yangu kwa msimu huu ni yapi, jibu langu sioni kama yapo, sina maana nikipata nafasi ya kufunga sitafunga ama kutoa asiti isipokuwa siwezi kusema nje na uhalisia nitafanya hiki na kile, hapana, labda hadi msimu ujao mambo mengi yatakuwa yamekaa sawa,” alisema mshambuliaji huyo.

Adebayor ambaye wakati anatua Singida Black Stars mwanzoni mwa msimu huu alikuwa akicheza AS GNN kwa mkopo kutoka Amazulu FC ya Afrika Kusini, mechi yake ya kwanza Ligi Kuu Bara ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons mzunguko wa kwanza.

Singida Black Stars ipo nafasi ya nne katika mechi 23 za Ligi Kuu Bara, imeshinda 13, sare tano, imefungwa michezo mitano ikikusanya pointi 44, jambo ambalo Adebayor anatamani kuiona timu hiyo inamaliza nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *