Mechi mbili kuamua hatma ya Samatta PAOK

CHAMA la Mtanzania, Mbwana Samatta limebakiza mechi mbili za kuamua hatma ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, ikisaka kumaliza katika nne bora Ligi Kuu ya Ugiriki ‘Super League’ msimu huu.

PAOK FC leo itashuka uwanjani kusaka pointi tatu dhidi ya Asteras Tripolis iliyopo nafasi ya sita ikiwa na pointi 35 ikiwa nyumbani kabla ya kumaliza mchezo wa mwisho dhidi ya Athens Kallithea ugenini Machi 9 na mechi zote ushindi ni lazima.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 14 zinacheza michezo 26 kila moja kwa mfumo wa nyumbani na ugenini na mwisho wa msimu timu nne za juu huchuana katika mtoano kwa michezo sita kila moja kuamua bingwa na zitakazofuzu Uefa.

Katika mechi 24 ilizocheza hadi sasa, PAOK ambayo ndiyo bingwa mtetezi, imeshinda 13, sare nne na kupoteza saba na matumaini yao ni kushinda michezo hiyo miwili kuanzia wa jana ili kujiwekea uhakika wa kufuzu UEFA.

Endapo isiposhinda michezo yote kuanzia wa jana, chama hilo la nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Samatta linaweza kushushwa na iliyo nafasi ya tano, Aris endapo itashinda mchezo wa mwisho baada ya juzi Jumamosi kutoka sare ya bao 1-1 hidi ya NFC Volos.

Katika msimamo wa ligi hiyo, unaongozwa na Olympiacos na pointi 54, ikifuatiwa na AEK Athens FC (52) na Panathinaikos (46), huku PAOK ikiwa nafasi ya nne na 43.

Baada ya mchezo wa jana Machi 09 itamaliza ugenini dhidi ya Athens Kallithea iliyopo nafasi ya 13 na pointi 18 na ikishinda hapo PAOK itajihakikishia kumaliza nafasi ya nne.

Katika mechi hizo PAOK ina nafasi ya kumaliza nafasi ya nne  kwani ikitumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuchukua pointi tatu dhidi ya Asteras na kumaliza kazi ugenini.

Samatta amekuwa na muendelezo wa kupata nafasi hivi karibuni  akifunga mabao matatu kwenye mechi nane alizocheza msimu huu ambao hakuanza vyema akisugua benchi.