KUNA mechi nne za kuchezesha karata ngumu. Ni lkesho jioni majibu yote yatapatikana. Mjadala mkubwa zaidi ukiwa kwa Yanga na KMC pale Mwenge, Dar es Salaam. Rekodi zinaonyesha kuwa mbaya kwa KMC kwani mechi 13 walizowahi kukutana na Yanga kwenye ligi imeambulia ushindi mara moja na sare mbili.
KMC watakaowakaribisha Yanga, ni mchezo mmoja kati ya minne inayopigwa Ijumaa hii, mwingine utachezwa kwenye Uwanja Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora kwa wenyeji Tabora United kuvaana na KenGold, wakati pale Sokoine jijini Mbeya Tanzania Prisons watapambana na Namungo huku Kagera Sugar ikiikaribisha Fountain Gate Dimba la Kaitaba mkoani Kagera.

KMC VS YANGA
KMC inaikaribisha Yanga kwenye mchezo huo kuanzia saa 10 jioni ambao utakuwa wa 13 kwao tangu KMC ilipoanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2018. Yanga wanashikilia rekodi ya kuifunga KMC mara 10 wakifunga mabao 21 huku wao wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano na kupoteza mchezo mmoja, sare zikiwa mbili.
Endapo KMC itashindwa kuifunga Yanga, basi itaendeleza uteja na furaha kwa Yanga baada ya mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania kuambulia suluhu hivyo kurejea kileleni na kuishusha Simba.
Kwenye makaratasi unaweza kusema ni mchezo mwepesi kwa Yanga kutokana na rekodi zao bora dhidi ya wapinzani wao hao lakini KMC imeonekana kuimarika kiasi fulani kufuatia mchezo uliopita kuichapa Singida Black Stars.
Katika kuimarika huko, KMC msimu huu imepunguza idadi ya mabao ya kufungwa na Yanga baada ya duru la kwanza kupoteza kwa bao 1-0, kutoka kichapo cha 5-0 na 3-0 msimu uliopita.
Timu hiyo ya Kinondoni chini ya Kally Ongala ambaye ameiongoza kwenye mechi saba tangu amekabidhiwa mikoba ya Abdihamid Moallin, ameshinda miwili, sare mbili na vichapo vitatu.
Kocha mpya wa Yanga, Miloud Hamdi huu utakuwa ni mchezo wake wa pili katika ligi kuiongoza timu hiyo baada ya kukabidhiwa mikoba ya Sead Ramovic, mchezo wake wa kwanza aliambulia suluhu dhidi ya JKT Tanzania ugenini.
Yanga ambayo imetoka kubadili benchi la ufundi, ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inapata pointi dhidi ya KMC ambayo inaendelea kujijenga chini ya Ongala na safu yake ya ushambuliaji kuanza kujipata baada ya mzunguko wa kwanza kuonekana kuyumba eneo hilo.
“Tumejiandaa na mchezo huu kama tulivyojiandaa na mchezo uliopita, tunawaheshimu wapinzani, tumewaangalia wapinzani ni wagumu sana, tunachohitaji ni kwenda kuchukua pointi tatu, nimejiunga na Yanga kwa lengo la kutwaa mataji sikufurahishwa na matokeo yaliyopita nimeiandaa timu vyema kuhakikisha inapata matokeo.
“Ili kupata ushindi lazima upambane kwelikweli, huwezi kushinda kirahisi. Hatuangalii kilichopita, kilichopo mbele yetu ni cha muhimu zaidi,”€ alisema Kocha Hamdi akizungumzia mchezo huo.
Ukiangalia KMC katika mechi 18 ilizocheza imeruhusu mabao 23 ikionyesha wazi kwamba eneo lao la ulinzi likiongozwa na Juma Shemvuni lina shida. Ikiwa eneo hilo lina tatizo, inakwenda kukutana na Yanga iliyofunga mabao 42 kwenye mechi 18, hivyo wana mtihani mkubwa unaowakabili.
Katika kulitambua hilo, Kocha wa KMC, Ongala, amesema: “Tunatambua kuwa tunaenda kukutana na timu ambayo ni bora, ina wachezaji wazuri eneo la ushambuliaji lakini pia ukuta wao ni imara kutokana na kuruhusu mabao machache, tumejiandaa kwenda kupambania pointi tatu.
“Hatukuwa na muda mrefu wa maandalizi kutokana na ratiba ilivyo, lakini kiujumla tumejiandaa vizuri kujituma na kupambana, dakika 90 za mchezo zitaamua nani anastahili kuibuka na ushindi, rekodi ya Yanga ipo vizuri, wana washambuliaji wazuri, tumejiandaa kupambana nao, hautakuwa mchezo rahisi.”
Yanga katika mabao yake 42, inaonekana kuwa hatari zaidi kipindi cha kwanza, mbali na hilo, pia imekuwa vizuri kutumia dakika 15 za kwanza hivyo wapinzani wao wanatakiwa kuwa makini.

TABORA VS KENGOLD
Huu ni mchezo mwingine utakaochezwa lkesho kwenye Uwanja Ali Hassan Mwinyi kuanzia saa 8 mchana, Tabora United itakuwa timu mwenyeji ikisaka mwendelezo bora wa ushindi baada ya kuzifunga Namungo 2-1 na Kagera Sugar 2-0.
Timu hizi zinakutana kwa mara ya pili baada ya duru la kwanza matokeo kuwa sare ya 1-1. KenGold imekuwa haina matokeo mazuri kwenye ligi msimu huu kufuatia kukusanya pointi tisa katika mechi 18 ilizocheza ikiendelea kushika nafasi ya mwisho wakati Tabora ni ya tano na pointi zake 31.

PRISONS VS NAMUNGO
Tanzania Prisons inarudi kwenye uwanja wake wa nyumbani ikiikaribisha Namungo mchezo ambao hautakuwa rahisi kwa wageni. Hiyo ni kutokana na rekodi ya Prisons kufanya vizuri mechi mbili za mwisho ilipocheza hapo ikishinda zote dhidi ya Pamba Jiji (1-0) na Mashujaa (2-1).
Timu zote hazipo vizuri kwenye msimamo zikipishana nafasi moja, Namungo ni ya 13 na pointi zake 18, wakati Prisons iliyokusanya pointi 17, inashika nafasi ya 14.

KAGERA VS FOUNTAIN GATE
Huo ni mchezo wa mwisho lkesho utakaochezwa saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Kaitaba, timu hizo zinakutana kesho zote zikitoka kupoteza mechi za mwisho. Fountain Gate ikiwa ugenini ilifungwa 2-0 na KenGold wakati Kagera Sugar ikichapwa nyumbani 2-1 na Tabora United.
Kwa upande wa Kagera Sugar utakuwa ni mchezo wa kulipa kisasi baada ya duru la kwanza ugenini kukubali kichapo cha mabao 3-1, pia timu hiyo inahitaji matokeo baada ya kupoteza michezo miwili na sare moja kwenye michezo mitatu iliyopita ikianza na kichapo dhidi ya Yanga ugenini (4-0), Singida Black Stars (2-2 ) na Tabora United (2-1).