Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), David Nchimbi amesema jukwaa la The Citizen Rising Woman limekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha na kuinua wanawake nchini Tanzania.
Amesema hayo leo Machi 7, 2025 wakati wa kongamano la jukwaa hilo linalofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na MCL kwa ushirikiano na Crown Media na wadau mbalimbali.
Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Amesema: “Katika kipindi cha miaka mitano jukwaa hili limekuwa mstari wa mbele kutambua, kuangazia, kusherehekea mchango wa wanawake katika uongozi nchini. Jukwaa hili linajikita katika kuhakikisha ujumuishwaji na ushiriki wa wanawake kwenye ngazi mbalimbali za uongozi na uamuzi.”
Amesema lengo la hayo ni kuleta matokeo chanya katika jamii na kukuza ushiriki wa wanawake ili kufikia uwiano wa 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi ifikapo mwaka 2030.
Nchimbi amesema ni wakati wa taasisi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi za uamuzi kwa sababu uongozi shirikishi huleta maendeleo endelevu, uchumi imara na jamii yenye usawa.
“Kupitia jukwaa la The Citizen Rising Woman tunajenga mazingira yanayowezesha wanawake kuibuka na kuharakisha kasi yao ya kuleta mabadiliko katika jamii wanazoishi. Tunaposherekea miaka mitano ya jukwaa hili tunajivunia safari yetu, tunatathmini mafanikio yetu na kuangazia hatua zinazofuata ili kuendelea kusukuma mbele ajenda ya usawa na ujumuishaji wa wanawake katika jamii na taasisi zetu,” amesema.
Amesema kipindi cha miaka mitano ya jukwaa hilo kimekuwa na simulizi zaidi ya 270 za wanawake waliofanikiwa, ikiwa ni pamoja na kutoa tuzo kwa taasisi 45 zinazofanikisha ajenda ya usawa wa kijinsia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Victor Mushi alisema uwepo wa Dk Biteko katika tukio hilo ni kielelezo cha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza azimio la kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, uchumi, kutengeneza mazingira wezeshi pamoja na sera zitakazoharakisha ufikiaji wa maendeleo endelevu kuelekea usawa wa kijinsia nchini Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Victor Mushi akizungumza leo Machi 7, 2025 wakati wa kongamano la jukwaa hilo linalofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na MCL kwa ushirikiano na Crown Media na wadau mbalimbali.
“Tulipoanzisha jukwaa hili mwaka 2021 tuliahidi litaangazia maisha na simulizi za safari za mafanikio za wanawake wa Kitanzania, nia yetu ilikuwa kuhamasisha ili jamii yetu ione faida ya ushiriki wa wanawake katika kuleta maendeleo.
“Jukwaa la The Citizen Rising Woman tangu awali lilinuia kuwakutanisha wadau wa mafanikio na maendeleo ya wanawake kutoka nyanja mbalimbali, lengo letu siku zote ni kutambua, kusherehekea na kuwezesha wanawake wa Kitanzania katika nafasi za uongozi na kufanya uamuzi,” amesema.
Mushi amesema kama ilivyo kaulimbiu ya MCL kuliwezesha Taifa, jukwaa hilo ni njia mojawapo inayotumika kuiwezesha jamii kwa kuangazia wanawake kama kundi mahususi.
“Katika maeneo 12 ya azimio la Beijing kuna eneo moja kubwa la kukuza ushiriki na uwakilishi wa wanawake kupitia vyombo vya habari, kama njia mojawapo ya kuwainua na kuwakwamua. MCL kupitia The Citizen Rising Woman tutachochea usawa wa kijinsia kwa kuwaweka wanawake kwenye kila jambo.
“Sisi wote ni zao la mwanamke, wengi tukitathmini safari zetu za maisha tunaona mchango wa wanawake katika kutujenga tukawa tulivyo, hivyo basi leo tusherehekee mafanikio ya wanawake na tufikirie miaka 30 baada ya Beijing, tunazidi kuweka mazingira wezeshi ili kufikia ndoto ya usawa wa kijinsia,” amesema.
Akizungumza katika kongamano la kuwahamasisha wanawake hasa kizazi cha sasa (Gen-Z), Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lindam Group, Zuhura Muro amesema hawana budi kujiamini kuwa wana uwezo.

Mkurugenzi wa Impact leadership academy Tanzania, Zuhura muro wa pili (kushoto) akichangia kwenye mjada wa The Risimg woman kuhusu namna ya kukuza fulsa kwa wanawake kwenye nyasha tofauti. Picha na Michael matemanga
Muro amesema lazima mwanamke ajiamini, awe na mtandao mpana, wafanye kazi kwa bidii katika sekta mbalimbali walizopo, bila ya kukatishwa au kujikatisha tamaa.
“Mfano mimi nilialikwa benki na sikuwa najua lolote kuhusu masuala ya benki wala mimi siyo mchumi, lakini nikasema naweza kwa kuwa wameniamini na nikaweza,” amesema.
Kaimu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN – Woman) Tanzania, Katherine Goffod amesema licha ya kuwapo mipango madhubuti inayolenga kuweka usawa wa kijinsia, lakini bado kuna pengo kubwa kati ya ahadi za sera na utekelezaji wake.
Katherine akizungumzia pengo lililopo amesema ni lazima kujiuliza ni kitu gani kinakwamisha katika kutimiza ahadi hizo.
“Moja ya changamoto kubwa tunazokabiliana nazo katika kila nchi ni masuala ya ufadhili, uwekezaji mkubwa wa kifedha katika usawa wa kijinsia. Hii inahusisha uwekezaji wa rasilimali za umma na binafsi ili kuhakikisha ahadi hizo zinageuka kuwa hatua za kweli,” amesema.
Amesema kwa Tanzania ipo dhamira ikiwemo ya kisiasa katika ngazi za juu kabisa za uongozi, lakini ni vema kujiuliza ni jinsi gani dhamira hiyo inatafsiriwa kuwa mabadiliko halisi ya sera na programu ambazo zina athari chanya kwa wanawake na wasichana katika ngazi ya jamii.
“Hapo ndipo tunakutana na changamoto ya mila na desturi kandamizi. Sasa, tunapaswa kujiuliza tutabadilisha vipi mifumo hii ya kijamii? Hili linahitaji uhamasishaji, mabadiliko ya tabia, uwekezaji wa mara kwa mara, mazungumzo ya kijamii na kushirikiana kwa karibu kati ya wadau mbalimbali,” amesema.
Wakili na mwanaharakati wa haki za kisheria na uwezeshaji wa jamii, Arafa Kikwete amesema ili kuweka usawa wa kijinsia nchini Tanzania yapo maeneo mawili ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na yote yameangukia katika suala la kisheria.
Amesema moja ya pengo lililopo ni ndoa nyingi za utotoni zinazoshuhudiwa nchini, kwani umri wa kisheria wa ndoa kwa wasichana ni miaka 14, jambo ambalo linahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuwe na uwiano kati ya umri wa mtu mzima na umri wa ndoa kwa wasichana.
“Kwa sababu, ikiwa msichana anafunga ndoa katika umri huo mdogo, si haki kwani hawana nafasi ya kumaliza hata elimu ya sekondari, hawafikii kidato cha nne,” amesema.
Amesema kuna umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanahamasishwa na kuelimishwa juu ya thamani yao, kwa kuwahimiza kutambua uwezo wao na kuwaonyesha kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa.
“Ni muhimu kuwapa ujasiri wa kusimama imara na kufanikisha malengo yao,” amesema.
Amesema changamoto nyingine ipo katika sheria ya uraia ambayo mwanamke akiolewa na mume wa kigeni, mume huyo hawezi kupata uraia wa Tanzania.