
Mbeya. Kada Chama cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Peter Msigwa amekosoa kampeni ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya “No Reforms No Election,” akisema ni mbinu za kukwepa uchaguzi.
Akizungumza kuhusu hali ya kisiasa nchini, Mchungaji Msigwa amesisitiza kuwa kabla ya kudai maridhiano na pande nyingine, Chadema wanapaswa kukubaliana wao kwa wao, kwani hadi sasa chama hicho kimeendelea kugawanyika baada ya matokeo ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho.
Machi 23 mwaka huu, Chadema chini ya Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu walizindua kampeni za chama hicho ikiwa ni No Reforms No Election’, Stronger Together na Tone Tone’ tukio lililofanyika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Akizungumza leo Machi 27 jijini Mbeya wakati wa mkutano wa hadhara, Mchungaji Msigwa amesema kampeni hiyo ni dalili za kukimbia uchaguzi mkuu akieleza kuwa CCM inahitaji ushindani wa kweli akiwataka kutokimbia.
Amesema maridhiano wanayotaka, wanapaswa kuridhiana wao na kukijenga chama kwani baada ya uchaguzi wao wamegawanyika wenyewe akieleza kuwa hawana uwezo wa kuifundisha CCM.
“Rais Samia (Suluhu Hassan) ameleta 4R kwa lengo la kutaka ushindani wa kweli, lakini Chadema wanataka kukimbia mechi kuweka mpira kwapani, huo mkakati wao ni dhaifu na umeshindwa kabla haujaanza.
“Hawana nguvu yoyote uwe wa rasilimalifedha, rasilimali watu wamegawanyika wenyewe tangu kumaliza uchaguzi wao, kwani kiongozi wao alihitaji kwanza kuweka usawa wa chama,” amesema Msigwa.
Kada huyo wa zamani wa Chadema, ameeleza kuwa alifikia uamuzi wa kuondoka katika ngome hiyo kutokana na kukosa haki na demokrasia, akieleza kuwa hawezi kuwa katika chama ambacho muda wote ni kupinga.
Hata hivyo, mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema) ameongeza kuwa hakuna asiyehitaji mabadiliko, akieleza kuwa CCM imefanya mabadiliko makubwa katika kuwafikia wananchi kimaendeleo.
Amesema hakuna mwenye hakimiliki ya kuongoza nchi badala yake wananchi ndio wenye mamlaka hiyo akieleza kuwa Chadema inag’ang’ania zaidi madaraka badala ya kuelezea changamoto na mahitaji ya wananchi.
“Maendeleo na mabadiliko yoyote ni mchakato, CCM imefanya makubwa sana, Chadema muda wote ni kupinga na kukazania madaraka, hakuna mwenye hakimiliki ya nchi zaidi ya wananchi, hawawezi kuelezea masuala ya wananchi ikiwamo kilimo na usafiri wa anga.
“Yapo mabadiliko yaliyofanyika tuliona uchaguzi uliopita wakurugenzi ndio walisimamia, lakini Rais anaweza kupigiwa kura maeneo yoyote tofauti na uchaguzi uliopita” amesema Msigwa.
Amewaomba wananchi kupuuza baadhi ya hoja za Chadema akiwataka kushiriki vyema uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.