Mchungaji Mono: Nilivyoona taarifa ya uteuzi wangu mtandaoni nilitokwa na machozi

Moshi. Askofu Mteule wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Daniel Mono amesimulia namna alivyopokea kwa mshtuko na machozi taarifa za kuchaguliwa kwake kuiongoza dayosisi hiyo, kumrithi mtangulizi wake, Askofu Chediel Sendoro.

Mchungaji Mono amepokewa leo Jumatatu, Machi 24,2025 katika dayosisi hiyo ya Mwanga, akitokea Shinyanga alikokuwa akihudumu. Amesema taarifa za kuchaguliwa kwake alizipata Machi 10,2025 kupitia habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, akiwa nchini Burundi.

Mchungaji Mono ambaye alikuwa Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya kusini Mashariki ya Ziwa Victoria-Shinyanga, (DKMZV) alichaguliwa Machi 10, 2025 katika mkutano mkuu maalumu ambapo alipata kura 127 za ndio sawa na asilimia 96.2, kati ya kura 132 zilizopigwa, huku kura za hapana zikiwa ni tano.

Mchungaji Daniel Mono akishuka kwenye gari, baada ya kuwasili Dayosisi ya Mwanga, ambapo amepokelewa leo, Machi 24, 2025.

Akizungumza na baadhi ya waumini na viongozi wa Dayosisi hiyo, katika Kanisa kuu la Mwanga, Mchungaji Mono ambaye leo amekabidhi ofisi tayari kuendelea na majukumu mbalimbali akisubiri kuingizwa kazini Julai 13,2025, amesema baada ya kuona taarifa za kuchaguliwa kwake, alishtuka na kutokwa na machozi.

“Ninamshukuru Mungu ajuaye yote, imempendeza kuniita kwa njia ya vyombo vya maamuzi vya dayosisi ya Mwanga kuja kutumika kama mtumishi wenu. Ni neema ya Mungu na  ninakiri kwamba mimi si bora kuliko wengine ila imempendeza Mungu kuniita nami nimepokea kwa unyenyekevu na utayari,” amesema mchungaji huyo.

Amesema halikuwa jambo rahisi alipopata  taarifa hizo akiwa Burundi katika  mjini Bujumbura.

“Nikiwa kule saa tano hivi, nikaona kwenye mitandao, kwa kweli ni jambo ambalo nililipokea kwa mshtuko na waliokuwepo ni mashahidi na leo Mungu amenitia nguvu,” amesena Mchungaji Mono.

“Nilipokea kwa machozi mengi na leo nikamuuliza Mungu mbona leo silii, akaniambia ulilia imetosha, hivyo nilipokea kwa unyenyekevu na shukrani, niwashukuru kwa mapokezi ya leo, sikuyastahili haya, Mungu ambaye mmemtendea haya apokee utukufu na hili liwe mbegu ya kuieneza injili katika eneo letu,” amesema.

Aidha mchungaji huyo ametumia nafasi hiyo kuwaomba waumini wa Dayosisi ya Mwanga kumuombea na kumpa ushirikiano katika kipindi ambacho amepewa kuwatumikia na  kuahidi kuendeleza yaliyoanzishwa na mtangulizi wake na kuanzisha mengine kwa utukufu wa Mungu.

“Mimi na wenzangu tutaendelea hapa kwenda mbele kwa sababu kuna kazi zinaendelea, tutaendelea kuzitekeleza kwa neema ya Mungu na Mungu atusaidie, na kadiri Mungu atakavyotujalia tutapanga pamoja kazi za nyongeza ziungane na hizo zinazoendelea ili kumpa Mungu utukufu na kupeleka mbele gurudumu la injili na maendeleo katika Dayosisi yetu,” amesema.

Naye Askofu wa Dayosisi ya Kati -Singida, Syprian Hilinti ambaye ni mlezi wa dayosisi hiyo tangu Askofu Sendoro afariki dunia, amewataka waumini wa Mwanga kumpa ushirikiano askofu huyo mteule pamoja na kumuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa utukufu wa Mungu.

“Huyu ameshushwa na Mungu kuja kutumika hapa, tuache habari za ukanda, hakuna waliowahi kuweka ukanda wakafanikiwa, tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano katika kuhakikisha kazi ya Mungu inasonga mbele,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jimbo la Shinyanga, Grayson Kinyaha amesema kazi alizozifanya Mchungaji Mono katika Dayosisi ya Shinyanga, zinaishi na wataendelea kumkumbuka.

“Mchungaji Mono amezaliwa Mwanga, lakini kihuduma amezaliwa kwetu Shinyanga, tunampenda na tutaendelea kumpenda kwa sababu kazi alizofanya zinaishi na kikubwa tutaendelea kumuombea kwa Mungu katika utumishi huu mpya alioitiwa”amesema Mchungaji Kinyaha.

Nao baadhi ya waumini wa Mwanga, Beatrice Charles na Angela Nelson wamesema wamekuwa wapweke kwa muda mrefu, lakini leo wamempokea baba ambaye ndiye askofu wa dayosisi hiyo na watampa ushirikiano mkubwa.

Dayosisi ya Mwanga ilifanya uchaguzi wa Askofu ikiwa ni miezi sita imepita tangu Askofu Chediel Sendoro afariki kwa ajali na hivyo nafasi hiyo kubaki wazi.

Askofu Sendoro ambaye alihudumu kama Askofu wa Mwanga kwa miaka minane, alifariki Septemba 9,2024 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Historia inaonyesha kuwa, Askofu Sendoro ndiye wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye  aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6,2016 baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare.

 Dk Mono ni Nani

Mchungaji Dk Daniel Mono, alizaliwa Julai 15,1975, wilayani Mwanga, akiwa ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya watoto saba.

Dk Mono baada ya elimu ya sekondari alipata elimu ya juu katika vyuo mbalimbali ambapo 2013 hadi 2018 alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Theologia (DMn) chuo kikuu cha Theologia cha Concordia cha Marekani.

Mwaka 2010 hadi 2012 alipata shahada ya Uzamili katika Theologia (MTh) katika chuo kikuu cha Tumaini Makumira na mwaka 2004 hadi 2009 alipata shahada ya kwanza katika theologia (BD) katika chuo kikuu cha Tumaini Makumira.

Mwaka 2000 hadi 2001 alipata Stashahada katika usimamizi na uongozi katika chuo kikuu cha Kimataifa cha Camridge, huku mwaka 2019 hadi 2022 akipata mafunzo ya uongozi wa Kilutheri chuo kikuu cha Theologia cha Concordia Marekani.

Alibarikiwa kuwa Mchungaji  Desemba 6, 2009 Kanisa Kuu Imani Mwanza Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria ambapo amefanya kazi katika nyanja mbalimbali na mwaka 2013 hadi 2017 alikuwa Katibu mkuu KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria.

Mwaka 2012 hadi 2022 alikuwa Mkuu wa Jimbo la Magharibi Kahama na Mchungaji Kiongozi Usharika wa Agape Kahama na Mkurugenzi Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Agape Kahama.

Desemba 2022 hadi sasa ni Msaidizi wa Askofu na mkurugenzi wa misioni, uinjilisti na uwakili Dayosisi ya kusini Mashariki ya ziwa Victoria (DKMZV).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *